Zaidi ya watu milioni 1.5 nchini Kenya wako katika hatari ya kukabiliwa na baa la njaa kufuatia kutokuwepo kwa mvua za kutosha.

Hali hiyo imewekwa wazi hivi karibuni baada ya waandishi wa habari nchini humo kuripoti tukio la njaa kwenye mji wa Turkana unaopatikana Kaskazini mwa nchi hiyo, ambao una asili ya ukame.

Aidha, baada ya habari hiyo kusambaa mitandaoni na kwenye vyombo vya habari, serikali ya nchi hiyo imekuwa ikikanusha kuwepo kwa hali hiyo, kwani imesema kuwa ilitoa shilingi bilioni mbili za ziada kuwapa Wakenya wapatao laki nane chakula na maji katika majimbo kumi na matatu yanayokabiliwa na baa la njaa.

Takriban majimbo kumi na matatu yako katika hatari ya kukabiliwa na baa hilo la njaa, maeneo hayo ni Turkana, Baringo, Pokot Magharibi, Marsabit, Wajir, Kilifi, Tana River, Samburu, Makueni, Isiolo, Mandera, Kajiado, Kwale na Garissa. Kati ya haya ni Turkana, Pokot Magharibi na Marsabit ambayo yameathirika zaidi na hata kushuhudia vifo.

Viongozi kutoka majimbo hayo wanaeleza kusuasua kwa serikali kuu na zile za majimbo katika kukabiliana na janga hilo la njaa, huku wengine wakiendelea kukanusha hali hiyo, na kusema hakuna Mkenya atakayekufa kwa njaa.

Hata hivyo Wakenya wengi wameitaka serikali kutopuuzia suala hilo, na kuendesha kampeni mitandaoni inayojulikana kama ##WeCannotIgnore ili kuhamasisha serikali.

Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Machi 20, 2019
Wimbo wa Vanessa watumika ligi ya kikapu Marekani

Comments

comments