Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta ameishangaza dunia hasa wale waliokuwa wakilimulika bara la Afrika kama bara lenye matatizo zaidi ya kutozingatia demokrasia, baada ya kuahidi ulinzi kwa wapinzani wanaompinga.

Akitoa ujumbe wake kwa wapinzani wanaopinga matokeo ya uchaguzi mkuu uliomuweka madarakani kwa muhula wa pili, Uhuru aliagiza jeshi la polisi nchini humo kuhakikisha linayalinda maandamano ya watu wanaopinga ushindi wake kwani yako kikatiba.

“Polisi wako tayari kuwalinda wakati mnafanya maandamano na wale waliochukia waelewe kwamba hawahitaji kibali changu wala cha Jubilee kufanya maandamano ya amani,” alisema Kenyatta.

Alisema maandamano ya amani ni haki ya Wakenya ya kikatiba kwa wale ambao hawakuridhishwa au wamekasirishwa na mchakato husika. Uamuzi huu huenda ukasababisha aandikwe kwenye rekodi ya vitabu maalum vya masuala ya demokrasia.

Kenyatta ambaye alitangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi uliofanyika Agosti 8 mwaka huu dhidi ya mpinzani wake mkuu, Raila Odinga amewataka waandamanaji kutovunja sheria kwa kufanya uharibifu wa mali au shambulio la kuwadhuru watu kwani Serikali yake haiko tayari kuona vitendo hivyo vikifanyika.

Katika hatua nyingine, Raila amewaahidi wafuasi wake kuwa leo atatoa tamko zito kuhusu nini ambacho wanapaswa kufanya kama sehemu ya kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu yaliyotangazwa na Tume Huru ya Uchaguzi ya IEBC.

HK Hyperman ‘kutia kachumbali’ ndoa ya Dulla Makabila na Husna
Zuma: misimamo yangu ilitaka kunisababishia kifo