Marais Joe Biden wa Marekani na Uhuru Kenyatta wa Kenya wamejadili uwazi wa kifedha katika mkutano wao uliofanyika Ikulu ya Marekani, wakati kiongozi huyo kutoka Afrika Mashariki akikabiliwa na uchunguzi kuhusu taarifa kuwa yeye na familia yake wameficha mamilioni ya dola katika akaunti za siri ughaibuni.

Kwa mujibu wa kituo cha habari cha Idhaa ya Kiswahili (DW) White House imesema viongozi hao wawili walisisitiza umuhimu wa kuongeza uwazi na uwajibikaji katika mifumo ya kifedha ya ndani na nje ya nchi.

Biden hakugusia madai hayo walipozungumza na waandishi wa habari lakini alitoa wito wa kuimarishwa kile alichokitaja kuwa “uwazi katika mifumo ya fedha.” Alimshukuru Kenyatta kwa uongozi wake wa kulinda amani, usalama na demokrasia ya nchi yake na kanda nzima.

Katika mkutano huo, Biden alitangaza ushirikiano katika vita dhidi ya janga la corona ambapo Biden na Kenyatta waliahidiana kufanya kazi pamoja kuhusu mabadiliko ya tabianchi na kumaliza machafuko katika pembe ya Afrika.

Hata hivyo Biden alitangaza kuwa Marekani itatoa mara moja msaada wa dozi milioni 17 ya Johnson & Johnson kwa Umoja wa Afrika, ikiwa ni nyongeza ya dozi milioni 50 ambazo ilishatoa ambapo ameahidi kutoa misaada zaidi ya chanjo dhidi ya COVID-19 kwa Kenya ifikapo mwisho wa mwaka.

“Ni furaha kusikia tangazo lako jipya la nyongeza hiyo ya chanjo kwa sababu kama mjuavyo, kama bara tunajikokota nyuma ya mabara mengine kuhusu uwezo wa kuwachanja watu wetu. Kwa hivyo nyongeza yoyote ya msaada kama ambavyo Rais Biden ametaja inakaribishwa sana na tunatumai kushirikiana zaidi,” amesema Rais Kenyatta.

“Nchi zetu zinashirikiana kwa dhati kuhakikisha kuna haki, heshima na usawa, na nimejitolea kuimarisha ushirikiano zaidi na Kenya nan chi za Afrika nzima- lakini Kenya ni mshirika muhimu kwa hili,” amesema Biden.

Kenyatta ndiye kiongozi wa kwanza wa Afrika kuzuru ikulu ya Marekani chini ya utawala wa Biden, mnamo wakati ziara na mikutano ya kilele imepunguzwa kama hatua ya kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona.

Kenyatta ni mmoja wa zaidi ya wanasiasa 330 wa sasa na wa zamani waliotambuliwa kuwa warithi wa akaunti za siri zilizofichuliwa katika ripoti za karibuni zinazofahamika kama Nyaraka za Pandora.

Bill Clinton alazwa ‘ICU’, daktari wake anena
Simba yashtukia hujuma Botswana