Rais wa Kenya ambaye ni mgombea wa nafasi hiyo kwa muhula wa pili, Uhuru Kenyatta ametoa ya moyoni baada ya mpinzani wake mkuu, Raila Odinga kutangaza kujiondoa kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi wa marudio uliopangwa kufanyika Oktoba 26 mwaka huu.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni eneo la Taita Taveta, Kenyatta alisema kuwa uchaguzi wa marudio nchini humo utafanyika hata kama Raila hatashiriki.

“Sasa hivi nasikia kuwa Raila amejitoa kwenye mbio za urais baada ya kuturudisha kwenye uchaguzi wa marudio ambapo shilingi bilioni 12 za Kenya zimetengwa kwa ajili ya maandalizi,” alisema Kenyatta.

“Ni haki yake kutoshiriki kwenye uchaguzi lakini pia tunataka kumwambia tunaendelea na uchaguzi kwa kuzingatia haki ya wananchi kumchagua kiongozi wanaemtaka. Ashiriki au asishiriki tutafanya uchaguzi,” aliongeza.

Rais Kenyatta alimkosoa Raila akieleza kwamba hakuna sehemu yoyote kwenye Katiba ya nchi hiyo ambayo inataja jina lake [Raila Odinga] kuwa ndiye anayepaswa kugombea nafasi ya urais, hivyo uchaguzi utaendelea.

Hayo yote yanatokana na uamuzi wa Raila kutangaza kujiengua kwenye mbio za uchaguzi huo hapo jana, baada ya Mahakama kutupilia mbali maombi ya Kambi ya NASA ya kutaka maafisa wa Tume ya Uchaguzi ya IEBC waliosimamia uchaguzi uliopita kutohusika kwenye uchaguzi wa marudio.

Mahakama ya Juu nchini humo ilibatilisha matokeo ya uchaguzi wa Agosti 8 mwaka huu baada ya kujiridhisha kuwa uligubikwa na vitendo vya udanganyifu.

Kwa mujibu wa matokeo ya uchaguzi huo, Kenyatta alishinda akimzidi Raila kura takribani milioni 1.4.

Country Boy kuja na albam yenye 'watu wazito'
Video: IGP Sirro amtangazia kiama Mange Kimambi, Siri ya Prof. Kitilia kubwaga manyanga ACT-Wazalendo

Comments

comments