Kwa mara ya kwanza, Rais Uhuru Kenyatta ameangazia siasa za mrithi wake, na kuweka wazi upande anaopendelea uchukue nafasi yake ya urais Agosti 9

Licha ya kuwa na mvutano na naibu wake William Ruto, Rais Kenyatta kwa muda mrefu zaidi amekuwa kimya, akitoa tu ishara zisizo za moja kwa moja kuhusu upande anaoegemea.

Hata hivyo, alipokuwa akikutana na baadhi ya viongozi kutoka eneo la Magharibi mwa Kenya siku ya Jumanne, Januari 25, katika Ikulu ya Nairobi, Uhuru aliashiria kwamba anamuunga mkono Kinara wa ODM Raila Odinga.

Gazeti la People Daily liliripoti kuwa Uhuru aliidhinisha urais wa Raila akisema taifa litakuwa katika mikono mizuri atakapoondoka mamlakani.

Huku akitetea uamuzi wake wa kushirikiana na kinara huyo wa ODM, Uhuru alisema kuwa alifanya mashauriano ya kina na nafsi yake huku akiongeza kwamba “yeye sio wazimu kumpuuza naibu wake.” “Mimi sio mwendawazimu eti niamke siku moja na kukaa na mtu ambaye nimemchukia karibu maisha yangu yote na nimpuuze naibu wangu mwenyewe. Je, mnadhani nilifikia uamuzi bila kuchunguza nafsi yangu? Nina sababu zangu na hivi karibuni nitawaambia Wakenya, lakini kwa wakati mwafaka,” Uhuru alisema.

Alisema kuwa kwa wakati ufaao, ataanza rasmi kampeni ya kumpigia kiongozi huyo wa ODM huku akibainisha kikosi kinachoongozwa na Ruto kilianza kampeni mapema, akidokeza kuwa hivi karibuni timu ya Azimio itajitosa uwanjani na hatimaye kupata ushindi.

“Waache waendelee na kasi yao. Lakini wajue kuanza mapema hakuwahakikishii ushindi. Wakati mwafaka ukifika mtaniona nikizunguka katika taifa nikipigia debe Raila,” Uhuru alisema.

Katika kongamano hilo hilo, Uhuru anasemekana kukerwa na viongozi wa ANC na Ford Kenya ambao walitangaza rasmi kuwa watashirikiana kikazi na naibu rais mnamo Januari 23. Hata hivyo, alisema bado atawashawishi Musalia Mudavadi na Moses Wetang’ula kuona kwamba wanaunga mkono vuguvugu la Azimio la Umoja ambalo kupitia kwao Raila anatafuta urais.

Viongozi hao wawili walifanya maafikiano Machi 2018 baada ya makabiliano makali ya kisiasa yaliyoshuhudiwa 2017, wakati kinara wa ODM alipopinga ushindi wa Uhuru.

Uchaguzi Kenya 2022:Muunganiko wa Ruto na Mudavadi una tija?
Ahmed Ally awatuliza mashabiki Simba SC