Rais Uhuru Kenyatta amewaalika wabunge wa mrengo wa Azimio la Umoja katika chakula cha mchana Ikulu leo.

Katika mualiko huo ambapo wanaoitwa “Tangatanga” wamefungiwa kutohudhuria, taarifa zinasema viongozi wa mirengo ya Jubilee na ODM tayari wamewaalika wabunge wanaounga mkono Azimio la Umoja kwenye kikao hicho cha Ikulu.

Duru za kisiasa nchini Kenya zinaarifu ajenda ya mkutano huo haikuwekwa wazi lakini wadadisi wanasema lazima ni kupanga siasa za mrengo huo.

Mwaliko huo unajiri wiki moja tu baada ya Azimio kupata ushindi bungeni wakati wa mjadala kuhusu vyama vya kisiasa ambapo waliangusha mapendekezo yaliyokuwa yamewasilishwa na watu wa karibu wa naibu rais William Ruto.

Naibu katibu wa chama cha Jubilee, Joshua Kutunny alisema kikao hicho ni muhimu sana ili upande wa Rais ujipange kisiasa.

“Umekuja wakati muafaka kwani tunahitaji kujipanga msimu huu wa siasa,” Kutuny alisema.

Mbunge wa Kieni Kanini Kega alisema wandani wa Rais hawawezi kukutana na wenzao kutoka mrengo wa UDA.

“Mkutano huo ni wale ambao wamekuwa wakiunga mkono Rais na ajenda zake. Hatutarajii kuwaona wabunge wa Tangatanga humo,” alisema Kanini.

Hata hivyo taarifa za ndani kwa ndani kutoka duru tofauti za kisiasa zinazofuatilia uchaguzi huo zinasema kuwa, Rais Uhuru amekuwa akionekana kujiandaa kumuunga mkono Raila Odinga kwenye uchaguzi wa urais mwaka huu.

Aliyekuwa gavana wa Kiambu William Kabogo alisema kinara wa ODM Raila Odinga ni mradi wa Rais Uhuru Kenyatta katika uchaguzi wa mwezi Agosti kwa kuwa Rais amekuwa akitoa ishara za mpango wake na wenye macho tayari wamesoma mwelekeo wa Uhuru.

“Huwezi kuficha tena kuwa Raila ni mbombea wa Uhuru, unafaa uone haya. Kama wewe ni mwanasiasa mwenye tajriba, haya unayaona tu. Nimeskia alikuwa kwenye birthdei yake, ni ishara gani ingine mnasubiri?” Kabogo alisema.

Kenya inatarajia kufanya uchaguzi mkuu mwezi Agosti mwaka 2022 ili kupata Rais mpya atakaechukua nafasi ya Uhuru Kenyatta ambae muda wake wa kuhudumu katika nafasi hiyo umekwisha.

Simba SC bingwa Mapinduzi CUP 2022
CAF: KIHARUSI CHA JOTO kilimvuruga Sikazwe