Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta ameuchambua utawala wake kwa kusema ulikuwa na nyakati zote mbili za mafanikio na majuto kwa miaka 10 aliyokaa madarakani kuwatumikia Wakenya na kuwaasa Wananchi wa Taifa hili kutowachagua Viongozi waongo.

Kenyatta, ameyasema hayo kupitia hotuba yake ya kila mwisho wa mwezi aliyoitoa kwa njia ya mahojiano katika vituo vyote vya televisheni na redio vilivyokuwa vikitangaza katika eneo la Mlima Kenya lenye wapiga kura wengi,ikiwa ni muda mchache kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9 wa nchini humo kufanyika.

Mahojiano hayo, yametafsiriwa na wachambuzi wa masuala ya kisiasa kuwa ni urushaji wa silaha ya mwisho dhidi ya Naibu wake, William Ruto ambaye amekuwa mhasimu wake katika kampeni za uchaguzi kutokana na kumnadi Mwanasiasa mkongwe Raila Odinga ili arithi kiti chake.

Eneo hilo, liliwahi kutumiwa pamoja kati ya Rais Uhuru na Ruto katika kuwahamasisha Wananchi wa mlima Kenya, waliojiandikisha kwa idadi kubwa zaidi ya wapiga kura mwaka 2017 walipokuwa wakiomba kuchaguliwa tena na Rais Kenyatta, ili kuboresha maisha ya Wakenya.

Hata hivyo, wakati wa kampeni zake Ruto amekuwa akisisitiza kwamba alikuwa naibu mwaminifu wa Rais Kenyatta, na kwamba hatua ya bosi wake kuunga mkono mpinzani wake mkuu, mpeperushaji bendera wa Azimio Raila Odinga, ilikuwa usaliti kwa watu walioandamana naye.

Kaunti tisa za Mlima Kenya, ambazo ni Nyeri, Kiambu, Murang’a, Kirinyaga, Embu, Tharaka-Nithi, Laikipia, Meru na Nyandarua kwa pamoja zina wapigakura milioni 4.7 na katika hotuba yake, Rais alikwepa kuwarejelea wagombea Odinga na Ruto moja kwa moja, lakini akawataka wapiga kura wa Mlima Kenya kufanya uamuzi wa busara Agosti 9, 2022.

“Sitaki kufanya kampeni kwa sababu kipindi hicho kimekwisha, lakini ninyi nyote mnajua msimamo wangu ulipo, mimi ni muumini wa mtu anayeangalia ustawi wa watu, sio masilahi yake binafsi,” alisema Rais Kenyatta.

Amesema, majuto yake pekee katika muongo wake wa uongozi ni kushindwa kwa BBI na kiwango ambacho propaganda na ufisadi umekita mizizi nchini humo, na kwamba hana majuto kuhusu kusalimiana na kusameheana na Odinga kwani kitendo hicho kilisaidia kupunguza hali ya wasiwasi kufuatia uchaguzi wa 2017 uliokuwa na utata.

Kesho, Agosti 9, 2022 Kenya itaamua hatma yake kisiasa kwa wananchi wake kupiga kura ya kumchagua Kiongozi ambaye wanadhani anafaa kuliongoza Taifa hilo kwa muhula unaofuata kwa kurithi kiti cha Rais anayemaliza muda wake Uhuru Kenyatta.

Wakulima waaswa kuzingatia kilimo chenye tija
Waziri Mstaafu afarijika kumuona Rais msibani