Mkami Shirima anayedaiwa kumpiga kwa gongo msichana ambaye ni msaidizi wake wa kazi za nyumbani maarufu kama dada, Salome Zakaria Hoya (18) na kumtesa kwa njaa hadi kufa amepandishwa kizimbani mkoani Arusha na kusomewa shtaka linalomkabili.

Mtuhumiwa huyo anadaiwa kutenda kosa hilo Machi 6, 2020 akiwa mkoani humo. Leo, Machi 13, 2020 amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Arumeru na kusomewa shitaka moja la mauaji, mbele ya Hakimu mkazi mfawidhi, Amalia Mushi. Hata hivyo, kesi hiyo iliahirishwa hadi Machi 26, 2020.

Anadaiwa kufanya ukatili huo kwa madai kuwa binti huyo alimuibia pesa kiasi cha shilingi elfu hamsini. Video iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii ilimuonyesha binti huyo akiwa kwenye chumba kilichotapakaa damu kutokana na kipigo kikali alichopigwa.

Aidha, alionekana mtu anayesadikika kuwa ndiye Bosi wake huyo akiwa ameshika gongo akimtaka binti huyo amueleze pesa ameiweka wapi.

Katika video hiyo, Salome alisikika kwa sauti ya chini akisema kuwa hela ameweka chini ya meza, jibu ambalo lilimkasirisha mwanamke huyo na ndipo alipoamua kumpigia simu mume wake na kumwambia amsamehe kwa atakachoenda kumfanya binti huyo.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho  Gambo, jana Alhamisi, Machi 12, 2020, aliwaongoza mamia ya waombolezaji na ndugu waliojitokeza kuaga mwili wa marehemu Salome (18) katika viwanja vya hosptali ya mkoa ya Mount Meru mkoani humo ulipokuwa umehifadhiwa.

Mwili wa marehemu Salome umesafirishwa kwenda kijijini kwao wilaya ya Manyoni mkoani Singida kwa ajili ya maziko.

VIRUSI VYA CORONA: Mambo muhimu ya kuzingatia kuepuka, hatua za kuchukua
Halima Mdee, Ester Bulaya warudishwa selo