Kesi ya kudai haki ya kuuaga mwili wa aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Geita, Alphonce Mawazo iliyofunguliwa katika Mahakama Kuu ya Kanda ya Ziwa itasikilizwa leo asubuhi.

Kesi hiyo iliyofunguliwa na mawakili watatu wa Chadema kwa niaba ya baba wa marehemu, Mchungaji Charles Kajiko chini ya hati ya dharura sana dhidi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza na Mwanasheria Mkuu wa Seriakali imepangiwa kusikilizwa na Jaji Lameck Mancha ili haki ya pande zote.

Kesi hiyo imevuta usikivu wa wananchi wengi ambapo mamia ya wananchi walifika katika mahakama hiyo jana kwa ajili ya kufuatilia kesi hiyo huku jeshi la Polisi likiwa limeimarisha ulinzi na mara kadhaa kuwatawanya wananchi waliokuwa eneo hilo, kitendo ambacho kililalamikiwa na wananchi hao wanaoaminika kuwa wafuasi wa Ukawa.

Wakili wa Chadema, John Mallya ameeleza kuwa jana mahakama ilisikiliza upande mmoja wa walalamikaji na kuwataka kutoa muda wa walalamikiwa kupitia nyaraka za kesi hiyo ili waweze kuwasilisha utetezi wao mapema leo asubuhi mahakamani hapo.

Viongozi wa ngazi za juu wa Chadema wakiongozwa na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe na aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho, Edward Lowassa wako jijini Mwanza wakidai haki ya kuuaga mwili wa Mawazo jijini humo na baadae kufanya mazishi mkoani Geita.

Jeshi la polisi mkoani Mwanza liliwazuia Chadema kuuaga mwili wa mawazo mkoani humo kwa sababu za marufuku ya kufanya mikusanyiko kutokana na tishio la kipindupindu.

 

 

Picha: Lowassa Awatembelea Waliookolewa Mgodini Baada Ya Siku 41, Atoa Mchango Wake
Julius Mtatiro afunga mjadala wa Ubunge wa Segerea