Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, jana iliutaka upande wa Serikali kuhakikisha inakamilisha upelelezi wake na kujiridhisha kabla ya kuwasilisha kesi dhidi ya mbunge wa Arusha, Godbless Lema.

Agizo hilo kwa upande wa Serikali lilitolewa mahakani hapo na Hakimu Mkazi, Augustino Lwizile baada ya Wakili wa Serikali, Blandina Msawa kudai kuwa bado hawajakamilisha upelelezi wa kesi hiyo, hivyo kuiomba mahakama kupanga tarehe nyingine.

“Kuna maelekezo yametolewa baadhi ya kesi watu wa mashitaka mnatakiwa kuzileta mahakamani kabla hamjakamilisha upelelezi. Lakini pia kuna kesi kama hizi zilizopo mbele yetu mnatakiwa kuzileta mkiwa tayari mmekamilisha upelelezi,”alisema Hakimu Rwizile bila kufafanua.

Lema anatuhumiwa kwa kumtolea maneno ya kashfa Mkuu wa Mkoa wa Arusha kupitia ujumbe mfupi wa simu. Ujumbe huo ulitajwa mahakamani hapo kuwa unasomeka “Karibu, tutakudhibiti kama Uarabuni wanavyodhibiti mashoga.”

Jana, Lema hakuweza kufika mahakamani hapo kutokana na sababu zilizotolewa na wakili wake, John Mallya kuwa alikuwa akihudhuria vikao vya Bunge mjini Dodoma.

Kesi hiyo iliahirishwa hadi Oktoba 12 mwaka huu.

 

Wanafunzi wamng’oa meno mwalimu, wamtuhumu kuwadhalilisha
Video: Waziri Mkuu apokea zaidi ya sh. bil. 1.4 kwaajili ya maafa tetemeko la Kagera