Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeahirisha Kesi inayowakabili viongozi wa ngazi za juu na Wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) leo, hadi Agosti 06, 2018 kwa kile kilichodaiwa kutofika kwa mshtakiwa namba 5 ambaye ni Ester Matiko.

Hayo yamesemwa na mmoja wa washtakiwa wa kesi hiyo ambaye ni Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa ambapo amesema kuwa, Matiko amepatwa na dharula yupo nje ya nchi ingawa hawajafahamu zaidi huko ameenda kufanya nini.

“Kesi yetu imeahirishwa kutokana na mshtakiwa mmoja kutokuwepo Mahakamani leo, amepata dharula amekwenda Nairobi nchini Kenya, kwa hiyo ikashindikana kusomewa maelezo, sisi wote ni binadamu unaweza ukapanga kitu lakini ikatokea dharula,”amesema Msigwa

Aidha, usikilizwaji wa kesi ya viongozi wa CHADEMA umekuwa ukiahirishwa mara kwa mara kutokana na baadhi ya washtakiwa kushindwa kufika Mahakamani kusikiliza kesi.

Hata hivyo, viongozi wanaokabiliwa na kesi hiyo ni pamoja na Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu wa chama hicho Dkt. Vicent Mashinji, Naibu Katibu Mkuu bara John Mnyika, Naibu katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu.

Wengine ni Mbunge wa Tarime vijijini, John Heche Mbunge Tarime mjini, Esther Matiko Mbunge wa Bunda mjini Ester Bulaya Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa pamoja na Mbunge wa Kawe Halima Mdee.

 

Mwingine Chadema ang'atuka na kujiunga CCM
Bwege: Zitto hana makosa, makosa ninayo mimi