Hatimae kocha Khalid Adam ameweka wazi maamuzi ya kuachana na Mwadui FC ambayo msimu huu haina mwenendo mzuri wa matokeo kwenye michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mwadui FC mwishoni mwa juma lililopita ilikubali kichapo cha mabao 5-0 dhidi ya Young Africans, Uwanja wa CCM Kambarage mkoani Shinyanga, hali iliyoibua sintofahamu kwa kocha huyo mzawa.

Adam amesema ameamua kuachana na timu hiyo kutokana na kubebeshwa lawama za timu kufanya vibaya, huku akiambiwa ni matokeo ya kufanya usajili wa wachezaji ambao hawana uwezo.

“Nimeambiwa kuwa nimesajili wachezaji ambao hawana uwezo, ndiyo maana napoteza mechi. Lakini mimi nilisajili baada ya kuona siku zinakwenda na hakuna pesa za kusajili.”

“Na timu hii haijasajiliwa hata na shilingi 10,000, nilichofanya ni kuita wachezaji kwenye majaribio, tukapata tuliowapata, tunashukuru Mungu ndiyo wametufikisha hapa.”

“Kocha unaweza kulaumiwa kama mahitaji yote kwa timu yanatekelezwa, hapa nilipo tangu msimu umeanza wachezaji wamelipwa mshahara wa mwezi mmoja tu na hata vifaa vya mazoezi ni tabu, timu nzima ina mipira sita wakati unatakiwa uwe na angalau mipira 40.” Amesema kocha Khalid.

Mwadui FC imekuwa timu pekee Ligi Kuu iliyokubali kufungwa mabao mengi, ilichapwa mabao 6-1 dhidi ya JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Mwadui Complex, Oktoba 25, mwaka huu, na Oktoba 30, ikabugizwa 5-0 dhidi ya Simba kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Biden athibitishwa rasmi na wajumbe
Mwanasheria Mkuu wa Marekani ajiuzulu