Kiungo wa klabu bingwa nchini Italia Juventus FC Sami Khedira ameonyesha kumuhurumia Bastian Schweinsteiger, kufuatia mazingira yanayomzunguuka katika kikosi cha Manchester United.

Khedira ameonyesha hali hiyo akiwa katika kambi ya timu ya taifa ya Ujerumani, ambapo amesisitiza kuwa maisha anayoishi Schweinsteiger huko Old Trafford hayastahili kutokana na mambo makubwa aliyowahi kuyafanya katika medani ya soka.

Kiungo huyo kutoka nchini Ujerumani, ameonyesha huruma kwa mchezaji mwenzake kutoka taifa la Ujerumani, ikiwa ni siku mbili zimepita baada ya Jose Mourinho kutoliwasilisha jina la Schweinsteiger huko UEFA kwa ajili ya michuano ya Europa League huku akimuweka kwenye kikosi cha wachezaji ambao watacheza ligi kuu ya England kwa msimu wa 2016/17.

Jambo lingine ambalo limeonyesha kumgusa Khedira ni hatua ya Schweinsteiger kuwahi kutakiwa kufanya mazoezi na kikosi cha wachezaji wa akiba katika kipindi hiki ambacho benchi la ufundi la man Utd linaongozwa na meneja huyo kutoka nchini Ureno, tofauti na ilivyokua kwa Louis Van Gaal.

“Ni vigumu kuamini kama yanatokea, lakini inaniumiza sana kumuona mchezaji mwenye hadhi kubwa akidhalilika kwa kiasi cha kushindwa kufikirika,”

“Japo unapaswa kutii maagizo yanayotolewa na bosi (meneja), lakini haitakiwi kufikia katika hali kama anayofanyiwa Schweinsteiger, tangu alipowasili Mourinho huko Old Trafford. ” Alisema Khedira

“Wakati mwingine inapaswa kufahamika upi uzito wa mchezaji pamoja na mipango ya klabu, na ndio maana mchezaji kama huyo alisajiliwa, lakini cha ajabu anaishia kudhalilika kwa sababu za mipango ya meneja?.” Alihoji Khedira

Kama ilivyokuwa kwa Schweinsteiger, Khedira aliwahi kupata majeraha ya mara kwa mara akiwa kikosi cha Real Madrid na kufikia hatua ya kucheza michezo 24 ya ligi ya nchini Hispania ndani ya misimu miwili, hali ambayo ilitoa msukumo kwa meneja wa wakati huo Carlo Ancelotti, kukubali kumuachia, na hatimae alijiunga na mabingwa wa Italia Juventus.

Khedira aliwahi kuahidiwa mkataba mpya akiwa Real Madrid, lakini kwa hali iliyokua inamkabili kwa wakati huo, aliona ni bora asake mahala pengine kwa ajili ya kubadilisha changamoto ya soka lake, jambo ambalo ameshauri lifanywe kwa Schweinsteiger, ili aangalie uwezekano wa kuihama Man Utd.

“Sitaki kuingia mzozo uliopo kati yake na meneja wa Man Utd, lakini ninashauri ni bora angepewa nafasi ya kuondoka na kuangalia uwezo wa kucheza soka lake kwa amani na utulivu, lakini sio kwa namna anavyochukuliwa kwa sasa.” Aliongeza Khedira

Cristiano Ronaldo: Zidane Ni Ufunguo Wa Mafanikio Ya Real Madrid
Raphael Varane Afichua Siri Ya Kukataa Ofa Ya Man Utd