Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi Taifa (UVCCM), Kheri James amewataka vijana wa CCM kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali kuanzia serikali za mitaa ili kuweza kuendelea kuwahudumia Watanzania kwa ufasaha.

Ameyasema hayo katika mkutano wa uzinduzi wa Kagera ya Kijani uliofanyika leo Julai 27, 2019 katika viwanja vya Kata ya Hamugembe Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera ambapo amewataka wazee kuwaachia vijana kuendeleza mapambano ya kukitetea chama kwasababu bado wana nguvu za kuwatumikia Watanzania.

Amesema kuwa kutokana na kazi kubwa inayofanywa na mwenyekiti wa CCM Taifa ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli Wanaccm wanayosababu ya kutembea kifua mbele maana kazi inaonekana kwa macho.

“Niwambie Wanakagera na Watanzania tumepata Rais sahihi kwa wakati sahihi, hivyo Wanaccm hatuna sababu ya kushindwa kuyaongelea anayo yafanya Rais wetu, tunajua wapo wanaopinga mambo yanayofanywa na Rais wetu ila mimi niwaambie ukiona mtu anampinga kama sio chizi atakuwa mkimbizi,” amesema Kheri James

Pia amesema kuwa lengo la umoja wa vijana kuanzisha mkakati wa rangi ya kijani ni kuhakikisha wananchi na wanachama wa CCM wanakijua chama chao kuanzia shinani hadi taifa chama kinashika dora kwa kuwaeleza wananchi kazi kubwa iliyofanywa na serikali ya Chama Cha Mapinduzi.

Aidha, Kheri amesema kuwa kati ya watu wanaopaswa kuiunga mkono serikali ni vijana kutokana na fursa mbalimbali ambazo serikali imewatengenezea katika ajira, biashara, sanaa pamoja mambo mengi ikiwemo mikopo.

“Vijana tunalo deni kubwa kwa serikali yetu, nitamshangaa kijana atakayekaa kijiweni na kuitukana serikali, tusiwe kama batoromeo kwa kukaa njiani na kuanza kuombaomba, nendeni halmashauri kuna mikopo kwaajili yenu, utakapokwama serikali itakukwamua naomba vijana tutumie fursa zilizopo,” amesisitiza Kheri.

Kwa upande wake mjumbe wa kamati ya utekelezaji wa umoja wa vijana Taifa, Joan Kataraia amesama kuwa mkakati huo wa Kagera ya kijani umewekwa mahususi kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa na kuwataka vijana wenye sifa kujitokeza kugombea.

Uzinduzi wa Kagera ya kijani ni mfululizo wa uzinduzi wa mkakati huo katika mikoa mingine ambapo viongozi wa CCM Mkoa Kagera watahakikisha wanausambaza mpaka kwa mwanachama mmoja mmoja.

Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Julai 28, 2019
CCM Kagera yakunwa na utekelezaji wa Ilani

Comments

comments