Kada wa Chama cha Mapinduzi CCM, Haider Hussein Gulamali ameshinda kesi iliyokuwa ikimkabili juu ya kutaka kumhonga shilingi milioni 2 Afisa Usalama wa Mkoa wa Singida, Kiseo Nzowa.

Kwa mujibu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Singida, kesi hiyo imetupiliwa mbali baada ya mashahidi wa upande wa mashtaka kushindwa kuwa na maelezo yanayofanana.

Uamuzi huo umetolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Consolata Singano ambapo amesema kuwa amezingatia ushahidi wa mashahidi 9 wa upande wa Jamhuri waliofika mahakamani hapo ambapo hakuna ushahidi unaomgusa Gulamali moja kwa moja.

Amesema kuwa katika ushahidi wao kila shahidi ametaja rangi tofauti ambapo mmoja ametaja Kaki, mwingine nyeupe, huku wa mwisho akitaja rangi ya Brown jambo ambalo mahakama imeshindwa kuelewa bahasha ipi ilibeba fedha.

Aidha, ameongeza kuwa hata hatua za ukamataji hazikuainishwa vizuri kwani hakuna mahali palipo onyesha pesa ziliwahi kutaifishwa hadi zilipofikishwa mahakamani, pia namna zilivyotunzwa mpaka kufikishwa kama ushahidi.

Katika kesi hiyo, miongoni mwa mashahidi ni Ofisa Usalama Mkoa wa Singida, Kiseo Nzowa anayedaiwa kupewa rushwa hiyo ambapo amedai anafanya kazi kwa mujibu wa sheria.

Hata hivyo, Shahidi huyo amedai kuwa Gulamali alimpa Sh. Mil 2 ili amsaidie kupitisha jina lake kwenye kinyang’anyiro cha ubunge wa Jimbo la Singida Kaskazini na kwamba yeye hakuwa Mjumbe Kamati ya Siasa Wilaya.

 

Video: Mradi wa umeme watikisa, waombewa na viongozi 13 wa dini, Lowassa atoa siri kutorudi CCM
Umoja wa wabangua Korosho wampongeza JPM