Serikali imeagiza kuboreshwa kwa huduma za afya katika Wilaya ya Tunduru katika kituo cha Mkasale ambacho kimebainika kuwa na huduma mbovu huku pia kikiwa na uchakavu kwenye majengo yake hali ambayo inaweza kuhatarisha usalama na afya za watumishi na wagonjwa wanaohudumiwa hapo.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri  wizara ya Afya, Jinsia, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto, Dkt. Hamis Kigwangalla wakati wa ziara ya kikazi ya ukagazi wa utekelezaji wa agizo la uboreshaji wa vituo vya afya katika kila Kata nchini lilitolewa Desemba 2016.

Kigwangalla ametoa miezi mitatu kwa mkandarasi wa Maji kuhakikisha anaingiza mifumo ya maji ndani ya kituo hicho na kuutaka uongozi wa  kijiji kushiriki katika kufanya usafi wa mazingira yanayozunguka kituo hicho cha Mkasale.

Aidha, amesema Serikali inaendelea na uboreshaji wa huduma za afya na kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma zenye ubora na kwa wakati na lengo la serikali ya awamu ya tano ni kupunguza kwa asilimia kubwa changamoto zinazoikabili wilaya hiyo  ikiwa ni pamoja na kupunguza vifo vya kinamama wajawazito na watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.

“Hata hivyo nawasihi wananchi tumuunge mkono Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa vita aliyoianzisha ya kulinda rasilimali za nchi yetu, kwani taifa limekuwa likiibiwa kwa muda mrefu sana ila umefika muda kuhakikisha kuwa rasimali za nchi zinatunzwa na kulindwa kwa ajili ya vizazi vijavyo.” amesema Kigwangalla

Hata hivyo, ameongeza kuwa ili mwananchi aweze kushiriki katika shughuliza uzalishaji ni lazima awe na afya njema na ili awe na afya njema ni lazima wananchi kwa kushirikiana na Serikali kuboresha vituo vya kutoa huduma za afya na kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi.

 

Tazama hapa matokeo kidato cha sita (ACSEE), ualimu (DSEE) na GATCE 2017
Video: Uongozi NHC wamgusa Waziri Mkuu, atoa pongezi kwa utendaji wao