Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Hamisi Kigwangalla ameagiza hospitali zote za umma nchini kuweka utaratibu wa kuzuia watu kuingia wodini na simu zenye kamera.

Kigwangalla ameweka wazi agizo hilo hivi karibuni kupitia akaunti yake ya Instagram, akitaka hospitali kuweka utaratibu wa kudhibiti upigaji picha ndani ya wodi ili kuepusha usumbufu na upotoshwaji aliodai unafanywa na baadhi ya wanaharakati na taasisi zisizo za kiserikali.

“Naagiza Hospitali zote nchini kudhibiti wageni kupiga picha wodini Kwa kufanya 1.) kuzuia kupiga picha mawodini 2.) kuweka utaratibu mzuri wa kuzuia simu za kamera mawodini. #Hapakazitu,” aliandika.

Agizo hilo lilikuja baada ya kusoma ujumbe wa mtu mmoja aliyeelezea kunyanyaswa kwa mgonjwa mmoja wa Seli nundu (Sickle cell) katika hospitali ya Muhimbili. Mtu huyo alieleza kuwa mgojwa huyo mwenye maumivu makali alionekana kupuuzwa na kutopewa matibabu kwa muda ndani ya hospitali hiyo, hivyo aliwataka Waziri wa Afya na Naibu wake kufuatilia na kuchukua hatua.

Naibu Waziri huyo alieleza kuwa baada ya kwenda katika Hospital hiyo kwa kufanya ziara ya kushtukiza na kufanya mahojiano na mgonjwa huyo alibaini kuwa madai hayo hayakuwa ya kweli kwani alipokelewa na kupewa matibabu stahiki.

Alilaani kile alichokiita baadhi ya taasisi zisizo za kiserikali kubeza jitihada za serikali na kueneza habari za uongo.

“Na kwamba, hata siku moja wanaharakati wasidhani wanaweza kuwa mbadala kamili wa Serikali, wao ni wabia muhimu na wanaisaidia Serikali kuutumikia umma (complementary efforts) na Siyo mbadala (alternative) wa Serikali. Kama wabia wakuu wa Serikali, wanaharakati wana wajibu wa kusema ukweli bila kuegemea upande wowote ule ili kulinda heshima yao na kulinda ‘relevance’ yao kwenye mfumo wa uongozi na utawala wa nchi,” aliandika.

Watumishi kuitwa majina saa 9 usiku kusaka waliokwepa kukesha na mwenge
Video: Zlatan Ibrahimovic alivyo dhihirisha ubora wake Man U