Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla ameeleza kumkubali Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Fatma Karume baada ya kukutana na kujadili mambo kadhaa.

Dk. Kigwangalla na Fatma Karume wamekuwa wakitofautiana mitazamo katika masuala mengi kwenye mtandao wa Twitter, hususan kuhusu siasa na sheria.

Kupitia mtandao huo leo, Dk. Kigwangalla aliweka picha zinazomuonesha akiwa na Rais huyo wa TLS ambapo ameeleza kuwa walikuwa na mazungumzo marefu jijini Dar es Salaam kuhusu mada mbalimbali, na kwamba amebaini kuwa ni mtu mwenye uelewa mpana.

“Shangazi ni mtu poa sana, mnyenyekevu, mvumilivu, msikivu, mwenye uelewa mpana sana wa mambo, na ana sababu zake kwenye kila analofanya. Tungeweza kuongea mpaka asubuhi kwa jinsi mada zilivyokuwa nyingi, nzito na ndefu. Kwa hakika tutakutana tena. Inshaallah,” ameandika.

 

Aidha, Fatma naye ametumia mtandao huo kueleza kuwa tofauti zao za kimtazamo siku zote hulenga katika kuitakia mema nchi lakini hazihusiani na Uzalendo.

Aliongeza kuwa mijadala ni muhimu na kwamba pasipo na majadiliano hakuna maelewano.

“Sote ni waTZ. Sote tunaitakia mema nchi. Tunatofautiana kwenye NJIA yakuchukua lakini sio kwenye UZALENDO. Sote ni WAZALENDO na DIALOGUE ni muhimu sana kwa sababu bila ya DIALOGUE hakuna maelewano kuna DHANA tu na DHANA ni FIKRA binafsi zilokosa CHANGAMOTO na haziwezi kubadilika,” ametweet.

Picha za mkutano wa wanazuoni hao zimepokelewa kwa mitazamo chanya na watumiaji wa mtandao wa Twitter, ambao wengi wametumia jina la ‘Shangazi’ analotumia Fatma kumbatiza Kigwangalla jina la ‘Mjomba’.

Marekani yaionya Uturuki kuhusu Wanamgambo wa Kikurdi 'Itasimulia'
Rais Magufuli asimamisha bomoa bomoa makazi holela, atoa mbadala

Comments

comments