Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla ameamua kurudisha kwa jamii kwa kujitolea kuwasomesha wanafunzi watano katika chuo cha Utabibu (Tabora Institute) pamoja na kuwasomesha watoto wasiojiweza katika jimbo la Nzega vijijini.

”Nimeamua kuwasomesha watoto 5 zaidi pale Nzega mjini pamoja na kusomesha watoto wasiojiweza katika jimbo la Nzega Vijijini”. Amesema Kigwangalla

Mbali na hayo Dkt Kigwangalla amesema atawakatia bima ya afya wakina mama na wazee wote ili wawe na uhakika wa kupata huduma ya afya na tayari ameanza mchakato wa kuwatambua watu wenye uhitaji huo.

“Nitawakatia bima ya afya wakina mama na wazee ili wawe na uhakika wakupata huduma ya afya, nimeshaanza mchakato wa kuwatambua watu wenye uhitaji na hivi karibuni nitatoa msaada wangu.”

Amesema hatua hiyo ni kama sadaka aliyoamua kuitoa kama namna ya kurejesha shukrani kwa Mungu kufuatia kunusurika katika ajali mbaya ya gari iliyopelekea kifo cha aliyekuwa mpiga picha wake.

”Matokeo ya ajali ile ingeweza kuwa mbaya zaidi kuliko haya niliyoyapata, sina la ziada bali ni kumshukuru mungu kwa kutoa sadaka”  Amesema Kigwangalla.

Dkt. Kigwangala amezungumza hayo katika moja ya mikutano yake katika jimbo la Nzega Vijijini.

Agosti 4 mwaka huu  Waziri Dkt. Hamisi Kigwangalla alipata ajali mbaya ya barabarani katika kijiji cha Magugu Mkoani Manyara baada ya gari lake alilokuwa akisafiria kupinduka na kupelekea kifo cha aliyekuwa Afisa Habari wake Hamza Temba.

Lukuvi apiga marufuku kudai kodi ya nyumba kwa miezi 6
Historia za wachungaji 7 na utajiri wao