Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Taifa imemteua Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Kenan Kihongosi kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi ( UVCCM).

Kenan ameteuliwa kushika nafasi hiyo iliyokuwa ikishikiliwa na Raymond Mangwala ambaye Juni 19, 2021 aliteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kuwa Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro.

Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka amesema leo Jumanne Juni 22,2021 Kamati Kuu ya CCM Taifa iliketi chini ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan.

Shaka amesema Kihongosi ni kiongozi mwenye uzoefu kwani ameanzia ngazi za chini kuanzia Uenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Iringa na pia mkimbiza Mwenge wa Uhuru.

Kenan Kihongosi amewahi kuwa Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Iringa mwaka 2017 na baadaye Kiongozi wa mbio za mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2019.

Juni 19, 2020 Kihongosi aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha na aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati Dkt. John Magufuli mpaka Juni 19, mwaka huu alipoteuliwa na Rais Samia kuwa Mkuu wa Wilaya ya Iramba, ambapo amehudumu kwa siku mbili pekee mpaka anateuliwa kuwa Katibu wa UVCCM Taifa.

Rais Samia kuhudhuria mkutano wa dharura SADC
Chris Brown kuchunguzwa na Polisi