Rais mstaafu, Dkt. Jakaya Kikwete amewataka wabunge wa vyama tawala barani Afrika kuhakikisha wanahoji, kuiwajibisha na kuikosoa Serikali pale wanapoona kuna sehemu haikufanya ipasavyo.

Dkt. Kikwete alisema kuwa wabunge wa vyama vya tawala wanapaswa kuhakikisha wanaikosoa Serikali pale wizara husika zinapofanya mambo ambayo ni kinyume na ahadi zilizowekwa kwenye ilani zao za uchaguzi.

Rais huyo mstaafu ambaye ana jukumu la kusaidia juhudi za kurejesha amani nchini Libya aliyasema hayo wakati akichangia katika mjadala wa mada iliyowasilishwa juzi na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afrika Kusini, Barney Pityana kuhusu Utawala Bora na Sheria.

“Ni kitu kizuri kwa wabunge hawa kuwa wanahoji pale kunapokuwepo na mgogoro katika sehemu moja barani Afrika. Na hili ni jambo muhimu kunapokuwepo utawala wa sheria unaozaa utawala bora,” alisema Dkt. Kikwete.

Aidha, Dkt. Kikwete alizitaka Serikali barani Afrika kutowachukuliwa wapinzani kama maadui bali kuhakikisha kuna utawala bora unaozingatia sheria.

Katika hatua nyingine, alivitaka vyama vya upinzani kujenga utamaduni wa kukubali matokeo pale vinaposhindwa katika uchaguzi unaofanywa kwa haki, uhuru na demokrasia.

Ofisi za IMMMA Advocates zateketea kwa moto
Qatar yawatimua wanadiplomasia wa Chad