Rais mstaafu wa awamu ya nne wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika harambee ya kukusanya fedha kiasi cha Sh. bilioni moja, kwa ajili ya ukarabati wa Shule ya Sekondari Lindi iliyoungua Julai 2016.

Taarifa hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi pindi akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam, amedai kuwa maandilizi ya harambee yamekamilika na yanatarajiwa kuhudhuriwa na wadau mbalimbali toka sekta ya elimu nchini.

“Kutokana na fedha tutakazokusanya, tumepanga ujenzi uanze wakati wowote. Zoezi hili litakwenda sambamba na mpango wa mkoa kuboresha mfumo mzima wa masuala ya elimu toka ngazi ya awali,” amesema Zambi.

Mkuu wa mkoa huyo amekiri kuwa mkoa wake ni mmoja kati ya mikoa inayofanya vibaya kwenye matokeo ya mitihani ya kitaifa, lakini amesema hatua zimechukuliwa kurekebisha hilo , ikiwamo kupima uwezo wa walimu.

Kwa upande wake, Ofisa Elimu wa Mkoa huo, Emmy Mchuchuri, alitaja changamoto zinazoukabili mkoa huo katika elimu kuwa ni miundombinu mibovu, uzembe wa walimu, utoro na kutokuwapo na chakula cha mchana shuleni.

Amesema ofisi yake imeanza kutekeleza maazimio ya wadau juu ya namna bora ya kuboresha elimu ndani ya mkoa huo, ikiwamo utoaji wa chakula cha mchana shuleni na mafunzo kwa walimu, ili kujenga uwezo wao wa ufundishaji.

Aidha ameongezea kuwa walimu watakaobainika kuwa na viwango vidogo vya ufundishaji watashushwa madaraja yao.

Ethiopia yachagua Waziri mkuu mpya
Kidumu alazwa akidaiwa kula sumu