Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amesema kuwa serikali imejipanga kuhakikisha vijiji vyote nchini vitakavyo pitiwa na mradi wa Bomba la mafuta la Afrika Mashariki EACOP kupatiwa umeme mapema kabla ya mradi huo kuanza.

Ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na DAR24 MEDIA mara baada ya kumalizika kwa kongamano la wadau wa mkoa wa Kagera manispaa ya Bukoba ambapo ameeleza kuwa nishati ya umeme ni nguzo muhimu katika mradi huo hivyo serikali itahakikisha umeme unasambaa kwa haraka iwezekanavyo katika maeneo yote ambayo mradi huo utapita.

Amesema kuwa kwa upande wa Kagera vijiji vyote ambavyo havijapata umeme tayari vimeshaingia kwenye mpango wa kusambaziwa umeme katika mpango wa REA awamu ya tatu ili kuhakikisha wananchi wanapata matunda ya serikali yao.

Aidha, Mgalu ambaye ni mlezi wa mkoa wa Kagera kwa upande wa Nishati amekiri kuwepo kwa changamoto mbalimbali mkoani humo ikiwemo maeneo mengi ambayo utekelezaji wa mradi wa REA awamu ya pili haukuweza kufika na sasa tayari wizara imeshaanza kuyafanyia kazi.

“Natambua Kagera kuna vijiji ambavyo havina umeme lakini mpango uliopo tupo tunatekeleza Rea awamu ya tatu katika vijiji 134 lakini tupo mbioni kuanza kutekeleza mpango wa Rea awamu ya tatu mzunguko wa tatu ambao utaanza mwezi wa saba, utaratibu uliopo ni kumalizia maeneo yote ambayo hayakufikiwa,”amesema Mgalu

Pia ameongeza kuwa gharama za kufungiwa umeme kwa wananchi wote wa vijijini ni shilingi elfu 27,000/= ambapo amesema kuwa baada ya Rea kumaliza mradi na kukabidhiwa Tanesco bei imekuwa ikipanda ambapo amesema hata kama mradi ukiwa umeshakabithiwa uungaji wa umeme utakuwa bei ile ile.

Video: Mwalimu shule ya msingi anaswa na silaha ya kivita, Bodi yatangaza sifa mikopo elimu ya juu
Benki ya CRDB sasa kuanzisha Islamic Banking