Madiwani wanne wa Halmashauri ya Geita waliochaguliwa kwa tiketi ya CCM waligeuza ukumbi wa kuapishwa kwa baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo kuwa ukumbi wa komedi kwa muda baada ya kushindwa kusoma viapo vyao kwa kutokuwa na uwezo wa kusoma kwa ufasaha.

Madiwani hao ambao sauti zao zilisambaa kupitia ‘whatsApp’ ndani ya muda mfupi na kuwa maarufu, walitajwa kwa majina ya Heche Mathias wa kata ya Nyakagomba, Khadija Joseph wa kata ya Nyamigota, Daudi Simeo wa kata ya Nyamboge na Sele Juma wa kata ya Nyamwilolelwa.

Tukio hilo lilitokea majira ya asubuhi wakati Mwenyekiti wa muda wa kikao hicho alipowakaribisha madiwani kusoma viapo vyao mbele ya hakimu mkazi wa mahakama ya Geita, Joseph William.

Mtindo wa usomaji wa madiwani hao mithili ya mwanafunzi wa ‘vidudu’ uliwavunja mbavu wahudhuriaji huku Mkuu wa wilaya ya Geita, Omari Mangochie na Mbunge wa jimbo la Geita, Joseph Musukuma wakishindwa kujizuia na kucheka kwa sauti.

Hata hivyo, zoezi hilo la uapishwaji lilikamilika licha ya kuchukua muda mrefu huku madiwani hao wakifanikisha kuziona herufi moja moja na kuziunganisha kukamilisha kiapo chao.

Nape awashauri Wanafunzi Vyuo Vikuu Kutumbua Majipu, Anusuru Mdahalo wa Hotuba ya Rais
Matokeo Rasmi ya Uchaguzi wa Arusha Mjini Yatangazwa