Walimu wa shule ya msingi Kianda iliyoko wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa wamelaani kitendo cha Afisa Elimu wa wilaya hiyo, Peter Fusi kumshambulia mwalimu mwenzao na kumpiga makofi mbele ya wanafunzi alipokuwa anafundisha hivi karibuni.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Flora Kipesha amewaambia waandishi wa habari kuwa tukio hilo la kudhalilisha limewasikitisha na wameamua kufanya mgomo ili kumshinikiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo kumchukulia hatua kali Afisa Elimu huyo.

Mwalimu Kipesha ameelezea mgomo huo kuwa ungechukua siku mbili pekee na utahusisha kutoingia darasani kufundisha lakini walimu hao wataendelea na kazi za kuandaa mitihani ya wanafunzi hao wakiwa ofisini. Ameongeza kuwa katika siku za mgomo huo, wanafunzi wataendelea kuingia darasani na kujisomea.

Alimtaja mwalimu aliyekutana na dhoruba hiyo ya kupigwa makofi kuwa ni Jacob Msengezi (25), anayefundisha masomo ya hisabati darasa la saba.

Mwenyekiti wa CWT Mkoa wa Rukwa, Hance Mwasajone jana alimkabidhi Mkuu wa Wilaya hiyo, Mathew Sedoyeka ushahidi wa kimaandishi kuhusu tukio hilo. Mkuu huyo wa Wilaya aliahidi kulifuatilia na kuchukua hatua stahiki.

 

Magufuli kuwagawia wananchi sukari bure
Wekundu Wa Msimbazi Kusubiri Hadi Msimu Wa 2017-18