Kilimanjaro Stars – Timu ya Taifa ya Tanzania Bara kesho Jumapili Desemba 3, 2017 itacheza na Libya katika mchezo wa pili wa michuano ya kuwania Kombe la CECAFA – linaloandaliwa na Baraza la Soka la Afrika Mashariki.

Mchezo huo utakaofanyika Uwanja wa Machakos, utaanza saa 10:00 jioni (1600h) mara baada ya mchezo wa kwanza kati ya Kenya ‘Harambee Stars’ na Amavubi ya Rwanda utakaoanza saa 8.00 alasiri (1400h) utakaofanyika Uwanja wa Kakamega.

Michezo hiyo kama ilivyo kwa michezo mingine katika michuano hiyo itakuwa mubashara kutoka Kenya kwenye vituo mbalimbali vya televisheni ikiwamo Azam TV ya Tanzania.

Kilimanjaro Stars tayari wana shime kutoka kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia na Kocha Mkuu wa timu hiyo, Ammy Ninje.

“Msidharau mechi,” alisema Dk. Mwakyembe wakati wa hafla ya chakula cha jioni ambako alitumia baraza hilo kuwaaga vijana hao akiwataka wachezaji wa timu hiyo kwenda Kenya kujitahidi iliyofanyika Novemba 29, mwaka huu.

Wachezaji waliko Kenya ni makipa Ramadhani Kabwili (Young Africans, Aishi Manula (Simba SC) na Peter Manyika (Singida United).

Walinzi ni Gadiel Michael (Young Africans), Boniphace Maganga (Mbao FC), Kelvin Yondani (Young Africans), Kennedy Juma (Singida United), Erasto Nyoni (Simba SC) na Mohammed Hussein (Simba SC).

Viungo wa kati ni Himid Mao ambaye ni Nahodha (Azam FC), Jonas Mkude (Simba SC), Hamis Abdallah (Sony Sugar/Kenya), Mzamiru Yassin (Simba SC), Raphael Daud (Young Africans), Shizza Kichuya (Simba SC), Abdul Hilal (Tusker/Kenya), Ibrahim Ajib (Young Africans) na Amani Kiata  wa Nakuru All Stars ya Kenya.

Washambuliaji ni Mbaraka Yussuph (Azam FC), Elias Maguri (Dhofar/Mascat, Oman), Daniel Lyanga (Fanja FC/Mascat), Yohana Mkomola (Ngorongoro Heroes) na Yahya Zayd kutoka Azam FC ya Dar es Salaam.

Benchi la Ufundi linaundwa na yeye Ninje ambaye ni Kocha Mkuu mwenye Daraja ‘A’ la Shirikisho la Mpira wa Miguu Ulaya (UEFA), Fulgence Novatus (Kocha Msaidizi), Patrick Mwangata (Kocha wa Makipa), Danny Msangi (Meneja), Dkt. Richard Yomba (Daktari wa timu), Dkt. Gilbert Kigadye (Daktari wa Viungo) na Ally Ruvu (Mtunza Vifaa).

Magazeti ya Tanzania leo Desemba 3, 2017
Rais Karia Ashinda Ujumbe CECAFA