Mchezo wa ligi kuu ya soka Tanzania bara mzunguuko wa 20 kati ya mabingwa watetezi Young Africans dhidi ya Mtibwa Sugar uliokua umepangwa kuchezwa Machi 03 katika uwanja wa Jamuhuri mjini Morogoro, umesogezwa mbele.

Bodi ya ligi imefanya maamuzi hayo, ili kuipa nafasi Young Africans kujiandaa vilivyo kuelekea katika mchezo wake wa ligi ya mabingwa barani Afrika dhidi ya Township Rollers kutoka Botswana utakaopigwa Machi 06 jijini Dar es salaam.

Kabla ya maamuzi hayo kuafikiwa na bodi ya ligi, uongozi wa Young Africans ulilalamikia ratiba ya ligi kuu kuwabana, hususan mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar ambao ulikua umekaribiana sana na ule wa Township Rollers.

Young Africans ilikuwa na kibarua cha kucheza na Mtibwa Sugar baada ya kukutana na Ndanda FC ambao watapamba nao kesho Jumatano mjini Mtwara, kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona.

Mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar utapangiwa tarehe nyingine

Wapinzani wa Young Africans katika michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika Township Rollers, kwa sasa wanaongoza ligi ya nchini kwao Botswana kwa kufikisha point 45, ili hali Young Africans wanashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi kuu ya soka Tanzania bara kwa kuwa na point 37.

Harufu ya kuondoka kwa Arsene Wenger yaanza kunukia
Neymar huenda akaikosa Real Madrid Machi 6