Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un ameonekana hadharani kwa mara ya kwanza, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Shirika la Habari la nchi hiyo ‘KCNA’ leo, Mei 2, 2020, wakati ambapo vyombo vya habari vya Magharibi vikieleza kuwa huenda alikuwa mahututi au amefariki dunia.

Kim hajaonekana hadharani kwa siku ishirini, hali iliyochochea tetesi zilizoenea kwenye vyombo vya habari hususan vya Magharibi, ikielezwa kuwa yuko mahututi baada ya kufanyiwa upasuaji wa moyo. Baadaye, ilielezwa kuwa huenda amefariki dunia.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa Kim amekata utepe na kufungua kiwanda kikubwa cha mbolea katika mji mkuu wa chi hiyo, Pyongyang, tukio lililofanyika Ijumaa, Mei Mosi, 2020.

KCNA imeripoti kuwa tukio hilo lilihudhuriwa na watu wengi ambao waliitikia kwa shangwe kuu baada ya kiongozi huyo kukata utepe kuashiria kufunguliwa kwa kiwanda hicho.

Imeelezwa kuwa aliongozana na maafisa waandamizi wa serikali akiwemo mdogo wake, Kim Yo Jong.

Jana, mmoja kati ya wapinzani wa Kim Jong-un aliyekimbia nchi hiyo, Ji Seong-ho alikimbia chocho cha habari cha Korea Kusini cha ‘Yonhap’ kuwa amepata taarifa kutoka kwa chanzo cha kuaminika kuwa kiongozi huyo alifariki dunia wiki iliyopita.

Alidai kuwa Serikali inaandaaa utaratibu wa siri wa kumrithisha nafasi hiyo dada yake na kwamba taarifa za kifo chake zingewekwa hadharani wikendi hii.

Usiri wa mahali alipo kiongozi huyo, ulitoa nafasi ya tetesi hizo kusambaa kwa kasi. Hata hivyo, kutokana na jinsi alivyojichimbia, hata Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo Aprili 30, 2020 kwa nyakati tofauti walionesha kutofahamu alipo.

“Hatujamuona. Hatuna taarifa yoyote ya kuwaeleza leo kuhusu Kim Jong-un, lakini tunafuatilia kwa karibu sana,” alisema Pompeo.

“Kuna hatari kuwa kutakuwa na njaa, uhaba wa chakula ndani ya Korea Kaskazini pia. Tunafuatilia kila kitu kwa karibu, kwakuwa hayo yote yana madhara katika mpango wetu, ambao ni kuhakikisha tunaondoa mpango wa nyuklia nchini humo,” Pompeo aliiambia Fox News.

Kwa upande wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Guterres aliwaambia waandishi wa habari kuwa hawana taarifa yoyote kuhusu hali ya kiongozi huyo.

“Sisi hatuna taarifa yoyote ya kinachoendelea kuhusu Kim Jong-un,” Guterres alikaririwa na vyombo vya habari.

Saa chache baadaye, Shirika la Habari la Korea Kaskazini lilitangaza kuwa Kim Jong-un ameishukuru timu ya wataalam waliojenga kituo cha utalii kipya na cha kisasa nchini humo. Lilieleza kuwa taarifa hiyo ilisainiwa na Kim mwenyewe.

Ikulu ya Korea Kusini ilikanusha taarifa zilizosambaa zikidai kuwa kiongozi wa nchi jirani, Korea Kaskazini, Kim Jong-un amefariki dunia au yuko mahututi baada ya kufanyiwa upasuaji wa moyo.

Moon Chung-in ambaye ni Mshauri Mkuu wa Rais wa Korea Kusini, Moon Jae-in kwenye masuala ya sera za nchi za nje, aliiambia CNN kuwa Serikali ya nchi hiyo ina uhakika kuwa Kim Jong-un ni mzima wa afya njema.

“Upande wa serikali yetu uko vizuri, Kim Jong-un yuko hai na ana afya njema. Amekaa katika eneo la Wonsan tangu Aprili 13, 2020. Hakuna mizunguko yoyote isiyo ya kawaida ambayo imeshashuhudiwa,” alisema Moon Jae-in.

Tetesi hizo pia zilifanikiwa kupata kauli ya Rais wa Marekani, Donald Trump ambaye alisema kuwa ingawa hafahamu alipo, anaamini yu mzima wa afya na anamtakia kila la kheri. Aliwaambia waandishi wa habari kuwa kwakuwa taarifa hizo zimeripotiwa na CNN hana imani nazo.

“Sijui, mimi nina uhusiano mzuri na yeye, sijui… kama ni kweli yasemwayo hiyo ni hali ngumu sana, lakini ninamtakia heri…. Tuna uhusiano mzuri. Nimeshasema na ninasema tena sasa hivi kama mtu mwingine angekuwa kwenye hii nafasi [ya Urais wa Marekani sasa hivi] tungekuwa vitani na Korea Kaskazini, na tulikuwa karibu kuingia vitani na Korea Kaskazini. Kwahiyo, ninamwambia Kim Jong-un ‘namtakia heri,” Trume aliwaambia waandishi wa habari, Aprili 23.

Chelsea kufuata nyayo za Arsenal, West Ham Utd

Luc Eymael kusajili saba young Africans

Mbaroni kwa kumfungia ndani mkewe na mnyororo
Chelsea kufuata nyayo za Arsenal, West Ham Utd