Korea Kaskazini wamethibitisha kupitia Shirika la Habari la Taifa (KCNA) kuwa kiongozi wa nchi hiyo, Kim Jong Un jana, Mei 4 alishuhudia zoezi la majaribio ya makombora.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, makombora kadhaa yamefyatuliwa kuelekea katika bahari ya Japan kutoka Rasi ya Hodo.

Imeelezwa kuwa Kim Jong Un aliagiza kufanyika kwa majaribio hayo kwa lengo la kuimarisha vikosi vyake tayari kwa uchokozi wa aina yoyote utakaojitokeza.

Uamuzi huo umekuja ikiwa ni miezi kadhaa tangu kuvunjika kwa mkutano wa pili kati ya kiongozi huyo na Rais wa Marekani, Donald Trump baada ya kushindwa kukubaliana kuhusu masharti ya kuondolewa vikwazo.

Kadhalika, yamefanyika ikiwa ni siku chache tangu Kim Jong Un atembelee Urusi na kufanya mkutano na Rais Vladimir Putin.

Trump ametuma ujumbe kupitia Twitter akieleza kuwa anaamini Kim hataharibu njia nzuri ya kuelekea kwenye uhusiano bora kati ya nchi hizo na kwamba hatavunja ahadi yake kwake.

“Ninaamini Kim Jong-Un atatambua kabisa uwezekano wa kupanda kwa kasi kwa uchumi wa nchi hiyo na hatafanya jambo lolote la kuharibu au kuumaliza. Anafahamu pia kuwa niko pamoja naye na hatataka kuvunja ahadi yake kwangu. Makubaliano yatafikiwa,” Trump ametweet.

Leo, shirika la habari la Korea Kaskazini limefafanua kuwa Kim Jong-Un amesisitiza kuwa nchi hiyo inapaswa kujiimarisha zaidi katika nyanja ya usalama, kisiasa na kiuchumi ili kukabiliana na vitisho au uvamizi wa aina yoyote.

Habari Picha: Dkt. Raphael Chegeni azungumza na Watanzania waishio Uingereza
Canelo ampiga Jacobs kutetea ubingwa wa dunia

Comments

comments