Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jon Un leo ameandika rekodi/historia ikiwa ni mara ya kwanza kujibu maswali ya waandishi wa habari wa kimataifa mbele ya Rais wa Marekani, Donald Trump.

Trump na Kim wanaendelea na mkutano wao wa pili wa kihistoria jijini Hanoi nchini Vietnam ambapo wamezungumza na waandishi wa habari punde walipokaa mezani.

Kim alijibu swali la mwandishi wa habari aliyetaka kujua kama kuna uwezekano wa kuruhusu kufunguliwa kwa ubalozi wa Marekani nchini kwake.

Awali, Kim kupitia kwa mkalimani wake alieleza kuwa asingependa kulijibu swali hilo, lakini Rais Trump aliweka msisitizo, “ningependa kusikia hilo jibu, ni swali zuri.”

Kim alijibu kwa ufupi, “ni kitu ambacho kinakaribishika. Ningependa tulijadili hilo faragha na Rais Trump.”

Baada ya jibu hilo, Trump alikazia akiliunga mkono kuwa ni wazo zuri sana na watalizungumzia kwenye mkutano wao.

Swali lingine ambalo lilionekana kuwa la msingi kuhusu mkutano huo lililoulizwa na mwandishi wa habari likimlenga Kim ni kutaka kujua kama ana nia ya kuachana kabisa na mpango wa silaha za kinyulia.

“Kama nisingekuwa na nia ya kutaka kuachana na silaha za nyuklia nisingekuwa hapa leo kwa ajili ya mazungumzo,” alijibu Kim Jong Un.

Jibu hilo lilimuinua Rais Trump ambaye alishindwa kuvumilia na kulipongeza, “hilo ni jibu zuri sana. Wow. Hilo linaweza kuwa jibu zuri zaidi ulilowahi kusikia.”

Viongozi hao watakuwa na mkutano wa siku mbili katika jiji la Hanoi kwa ajili ya kujadili uhusiano kati ya nchi zao pamoja na mpango wa kuondoa silaha za kinyuklia katika Rasi ya Korea.

Mkutano huo ni muendelezo wa majadiliano ya mkutano wa kwanza kati yao uliofanyika Singapole mwaka jana.

Breaking: Mkutano wa Trump na Kim Jong Un wavunjika
Trump, Kim Jong Un uso kwa uso Vietnam