Kim Kardashian jana mchana alifanya mazungumzo na Rais wa Marekani Donald Trump ndani ya Ikulu ya ‘White House’.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na vyanzo vya kuaminika, Kim Kardashian ambaye ni mke wa Kanye West, alizungumza na Rais Trump kuhusu uwezekano wa kutoa msamaha kwa bibi mwenye umri wa miaka 63 anayetumikia kifungo jela.

Kikongwe huyo anayefahamika kwa jina la Alice Marie Johnson amekaa jela kwa zaidi ya miongo miwili akitumikia adhabu aliyopewa baada ya kukutwa na hatia ya kujihusisha na madawa ya kulevya.

Mkwe wa Trump ambaye pia ni mshauri wake, amekuwa akifanya mazungumzo mara kwa mara na Kim Kardashian kuhusu suala hilo.

Kim Kardashian, akiwasili Ikulu ya Marekani

Baada ya mkutano huo, Rais Trump alitweet, kwa tafsiri isiyo rasmi “Nilikuwa na mkutano mzuri na Kim Kardashian leo, tumezungumza kuhusu mageuzi kwenye masuala ya magereza na vifungo.”

Kim aliondoka Ikulu akiwa ndani ya gari lenye vioo vyeusi akikwepa kamera za mapaparazi waliokuwa wamefurika maeneo hayo, ingawa tayari alikuwa amenaswa kwenye picha zinazomuonesha alipokuwa akiwasili.

Picha rasmi za mkutano wa Kim na Trump zilitolewa na Ikulu.

Mume wa Kim Kardashian, Kanye West amekuwa akimuunga mkono waziwazi Rais Donald Trump na kuweka wazi kuwa msimamo wake unaungwa mkono pia na familia yake.

Zawadi 5 muhimu unazoweza kutoa kuelekea siku ya kina baba duniani
Mhubiri awaomba waumini wamnunulie Ndege