Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars Kim Poulsen ameelezea mikakati ya maandalizi ya kikosi chake kuelekea kwenye michezo miwili ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya timu ya taifa ya Kenya ‘Harambee Stars’.

Timu zote mbili zitatumia michezo hiyo kama sehemu ya maandalizi kwa ajili ya michezo ya kufuzu AFCON, itakayocheza baadae mwezi huu.

Poulsen amesema anazingatia zaidi kwenye mbinu za kushambulia na kujilinda ili kuweka uwiano sahihi kuelekea mechi za kufuzu.

“Mazoezi yetu, tunazingatia zaidi jinsi ya kushambulia na kujilinda kwa sababu unahitaji kuvitumia vyote kwenye mechi” Amesema Poulsen.

Poulsen pia ameelezea mipango iliyopo kwenye michezo miwili ya kimataifa ya kirafiki itakazochezwa huko mjini Nairobi, Kenya.

“Kwa sasa tuna wachezaji 23 kwenye kikosi na tunategemea kuwatumia kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Kenya utakayochezwa Machi 15, kundi la wachezaji wengine watacheza mchezo wautakayochezwa Machi 18”

“Naamini baada ya hapo tutakuwa na kikosi kamili kwa ajili ya kupambana kwenye michezo miwili muhimu dhidi ya Equatorial Guinea na Libya ili kufuzu kucheza fainali za AFCON”

Taifa Stars ipo kundi J kwenye mbio za kufuzu kwenda AFCON, ikiwa na alama 4, na inahitaji kukusanya alama nyingine zaidi ili kufuzu.

Viongozi wa kundi, Tunisia wameshafuzu baada ya kukusanya alama 10 kwenye michezo minne. Equatorial Guinea wapo nafasi ya 2 wakiwa na alama 6 na Libya wanashika mkia wakiwa na alama 3.

Wachezaji walioitwa kambini kwa ajili ya michezo hiyo ya kuwania kufuzu Fainali za Afrika (AFCON 2021): Aishi Manula, Metacha Mnata, Juma Kaseja, Shomari Kapombe, Hassan Kessy, Israel Mwednwa, Erasto Nyoni, Dickson Job, Bakari Nondo Mwamnyeto, Kelvin Yondan, Carlos Protas, Laurent Alfred, Kennedy Juma, Mohammed Hussein, Nickson Kibabage  na David Bryson.

Wengine ni Yassin Mustapha, Edward Manyama, Simon Msuva, Hassan Dilunga, Mzamir Yassin, Jonas Mkude, Saidi Ndemla, Fiesal Salum, Himid Mao, Ally Msengi, Baraka Majogoro, Salum Aboubakar, Iddy Nado, Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu  na John Bocco.

Pia wapo Yohanna Mkomba, Shaban Chilunda, Ditram Nchimbi, Deus Kaseke, Abdul Suleiman, Kelvin Pius John, Nassor Hamoud na Meshack Mwamito.

Mukoko amlilia Kaze, awapa kazi wachezaji
Namungo FC kucheza viporo VPL