BENCHI la Ufundi la Azam FC limeridhishwa kwa kiasi kikubwa na viwango vya wachezaji wa timu hiyo, wanavyovionyesha wakiwa na timu zao za Taifa katika michuano ya Kombe la Chalenji inayoendelea kutimu vumbi nchini Ethiopia.

Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, ameuambia mtandao wa azamfc.co.tz kuwa amekuwa akiiangalia michuano hiyo kupitia televisheni na kuwafuatilia kwa kina wachezaji wake 12 wanaoshiriki.

“Naifuatilia mechi kupitia televisheni, Khamis Mcha ‘Vialli’ alifunga bao jana (juzi) kwa Zanzibar, Bocco ameifungia pia Tanzania (Kilimanjaro Stars), Himid Mao alipata majeraha madogo akiichezea Tanzania.

“Tunaangalia mechi na kuangalia maendeleo yao, tunaangalia kama kuna iliyepata majeraha, tunaangalia utendaji wao wa kazi mzuri. Aishi Manula akiwa langoni, amefanya vizuri sana akiwa na Tanzania, nimemuona Allan Wanga akicheza Kenya kwa muda mchache, pia Kavumbagu (Didier) akicheza Burundi, hivyo tunaangalia mechi zote na kuangalia fomu za wachezaji, ufiti wao, viwango vyao ni jambo la msingi sana,” alisema.

Hall aliongeza kuwa Kilimanjaro Stars imecheza vizuri sana mpaka sasa kwenye michuano hiyo na akasema kuwa inao uwezo wa kulitwaa kombe hilo, ambapo leo itacheza tena na Ethiopia katika mchezo wa robo fainali.

Azam FC ni miongoni mwa timu ambazo zimetoa wachezaji wengi wakiwa na timu tofauti kwenye michuano hiyo na wengi wao wakifanya vizuri akiwemo nahodha John Bocco, aliyefunga mabao mawili, Didier Kavumbagu, amefunga bao moja licha ya timu yake kuishia hatua ya makundi na Khamis Mcha akiifungia Zanzibar bao moja.

Jumla ya wachezaji wanne kati ya 12 wa Azam FC waliokuwa kwenye michuano hiyo wanatarajia kurejea mazoezini Azam Complex muda wowote kuanzia sasa, baada ya mataifa yao kutolewa, ambao ni Ame Ally ‘Zungu’, Mcha, Mudathir Yahya ‘Muda’ na Kavumbagu.

Watakaoendelea kukosekana kwenye mazoezi ni John Bocco ‘Adebayor’, Himid Mao ‘Ninja’, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Shomari Kapombe, Aishi Manula (Kilimanjaro Stars) na Allan Wanga (Kenya) na Jean Baptiste Mugiraneza ‘Migi’ (Rwanda)

Watatu Watajwa Tuzo Ya Mchezaji Bora Wa Dunia 2015
Kobe Bryant Atangaza Kuachana Na B.Ball