Mabingwa wa soka nchini Ujerumani FC Bayern Munich, wataanza msimu wa 2016/17 bila ya kuwa na mshambuliaji wao wa pembeni kutoka Ufaransa Kingsley Coman, baada ya kupata majeraha ya kifundo cha mguu wakiwa katika maandalizi ya mwisho kabla ya kuanza kwa mshike mshike wa Bundesliga Agosti 26.

Coman, alijiunga na FC Bayern Munich mwezi Agosti mwaka 2015 kwa mkopo akitokea kwa mabingwa wa soka nchini Italia Juventus.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 20, alishindwa kuendelea na mazoezi ya kikosi cha FC Bayern Munich na kutolewa nje ya uwanja kwa gari maalum, kufuatia maumivu makali ya kifundo cha mguu yaliyomkabili.

Taarifa za awali zimeeleza kuwa, Coman, amepatwa ameumia vibaya sehemu za kifundo cha mguu wake wa kushoto na huenda akawa nje ya uwanja kwa muda wa majuma manne hadi manane.

FC Bayern Munich, wataanza kutetea ubingwa wa Bundesliga mwishoni mwa juma lijalo kwa kupambana na Werder Bremen, katika uwanja wa Allianz Arena.

Msimu uliopita Coman alikuwa mmoja wa wachezaji waliofanikisha furaha kwa mashabiki wa FC Bayern Munich pale walipotwaa ubingwa wa kombe la Ujerumani pamoja na ligi.

Uwezo wake wa kisoka tangu alipojiunga na mabingwa hao, umeanza kuwavutia viongozi wa FC Bayern Munich na tayari mtendaji mkuu Karl-Heinz Rummenigge ameshaanza kulipa sehemu ya fedha za usajili wake wa moja kwa moja, ambapo mpaka sasa ameshatoa kiasi cha Euro milioni 21 (sawa na Pauni milioni 18.1).

Msimu uliopita Coman alifunga mabao sita na kutoa pasi za mwisho 12 katika michezo 35 aliyocheza chini ya utawala wa meneja aliyeondoka Pep Guardiola.

Katika mchezo wa German Supercup ambapo FC Bayern Munich walipambana na Borussia Dortmund mwishoni mwa juma lililopita na kupata ushindi wa mabao mawili kwa sifuri, meneja wa sasa Carlo Ancelotti alimtumia Coman kama mchezaji wa akiba.

Coman ameshaitwa kwenye kikosi cha Ufaransa mara sita na alicheza mchezo wa hatua ya fainali ya michuano ya Euro 2016 kwa kuingia uwnajani katika muda wa nyongeza, baada ya wenyeji kufungwa bao moja na Ureno.

Patrick Hickey Akamatwa Na Jeshi La Polisi Nchini Brazil
Mario Gomez Arejea Nyumbani, Vurugu Za Kisiasa Zamkimbiza Uturuki