Kada mkongwe wa Chama Cha Mapinduzi, Kingunge Ngumbale Mwiru amesema kuwa Kamati ya Usalama na Maadili ya chama hicho ilikiuka katiba za chama hicho katika kuyachuja majina ya wagombea waliowania nafasi ya kupeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mkuu.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mzee Kingunge alisema kuwa kamati hiyo hiyo haikuzingatia maadili ya chama katika utendaji wake wa kazi na kwamba iliingilia kazi ya Kamati Kuu ya Chama hicho kwa maslahi binafsi.

Kingunge ameeleza kuwa kwa mujibu wa taratibu na kanuni za chama hicho, Kamati ya Usalama na Maadili hufanya kazi ya kuyapitia majina yote ya wagombea yaliyowasilishwa kisha kutoa mapendekezo kwa Kamati Kuu ambayo hutumia mapendekezo hayo kuamua majina matano ya kuyapigia kura kupata majina matatu.

“Kitendo hicho cha kuinyang’anya Kamati Kuu kazi yake si cha kawaida, ni uvunjifu wa taratibu na hakuna uadilifu ndani yake. Naiita kamati ya maadili, yenyewe inavunja maadili. Kwa sababu maadili ya chama yanaanzia kwenye kuheshimu muundo wa chama, sera za chama na taratibu zake. Kamati kuu inapelekewa orodha ya watu watano wapitishwe, hawa watu waliogombea wote hao 38 hawakuwaona, hawakuwauliza maswali, hawakupita mbele yao. Na hata huko kwenye Kamati ya Maadili naamini hawa wagombea hawakuitwa huko wakaulizwa maswali.

“Kwahiyo, kuna mahali watu fulani wachache wamekaa wakatengeneza orodha yao. mzee Amani Abeid Karume alisema ‘nchi hii ni yetu wote’. Na mimi nasema msemo huo maana yake tuliowapa madaraka wasifike mahali wakasema nchi hii ni yao wao, yale madaraka ni dhamana tu, wenyewe ni wananchi, wote watanzania.”
Kingunge ambaye ni mmoja kati ya wanachama wa kwanza wa chama hicho akiwa na kadi namba 8, alimtetea mbunge wa Monduli, Edward Lowassa na kudai kuwa sakata la Richmond lilimpa ushindi yeye kwa sababu serikali ilibainisha kuwa hakuwa anahusika moja kwa moja na kwamba yeye alihusika kisiasa tu.
Kingunge aliainisha kuwa Kamati ya Usalama na Maadili iliyo kuwa chini ya mwenyekiti wa chama hicho, rais Jakaya Kikwete ilikiuka katiba ya chama kwa maslahi binafsi ili kuliondoa jina la Edward Lowassa aliyedai anakubalika zaidi katika chama hicho.

Mchakato wa kumpata mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu ulimalizika July 12 ambapo Dkt. John Pombe Magufuli alitangazwa kuwa mshindi.

Migi Rukhsa Kuitumia Azam FC Kagame Cup
CUF Wazungumzia Taarifa Za Kujitenga Na UKAWA