Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-Un amemkejeli Rais wa Marekani, Donald Trump saa chache baada ya kufyatua kombora zito ambalo linadaiwa kuwa na uwezo wa kufika Marekani na sehemu nyingine duniani.

Timu ya ujasusi ya Marekani ilieleza kuwa kombora hilo la Korea Kaskazini lililofyatuliwa wiki hii limeonesha kufanikiwa kwa kiasi kikubwa na kwamba lilienda umbali wa zaidi ya Kilometa 900 kabla halijatua baharini kwenye eneo muhimu la kiuchumi nchini Japan.

Kwa mujibu wa Sky News, Kim Jong-Un ameeleza kuwa kombora hilo lililofyatuliwa Julai 4, siku ya kuadhimisha uhuru wa Marekani, lilikuwa zawadi yake kwa Marekani na kiongozi wake.

“Lilikuwa lenye muonekano wenye mvuto kama mvulana mtanashati,” Sky News inamkariri Kim Jong-Un. “Ilikuwa zawadi nzuri kwa Marekani siku ya maadhimisho ya uhuru wao,” anadaiwa kuongeza.

Taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Marekani imeeleza kuwa Rais Trump na timu ya wana usalama inaendelea kuvifanyia usaili wa karibu vitendo vya Korea Kaskazini na kwamba nchi hiyo imefikia ukomo wa uvumilivu wake.

Imeeleza kuwa Marekani itaongeza vikwazo zaidi dhidi ya nchi hiyo wakati ambapo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likitarajiwa kujadili hatua dhidi ya Korea Kaskazini.

Urusi na China, jana zilitoa tamko la kulaani majaribio ya makombora yanayofanywa na Korea Kaskazini, ambayo ni tishio kwa dunia nzima.

Lipumba atangaza mkakati wa CUF kusaidia kukomesha mauaji Kibiti
Halima Mdee Akamatwa, Atupwa Selo