Afisa mtendaji mkuu wa Namungo FC Omar Kaaya pamoja na wachezaji watatu wa klabu hiyo Lucas Kikoti, Fred Tangalu na Khamis Faki waliokua wamewekwa ‘KARANTINI’ nchini Angola, ameruhusiwa kurejea Tanzania.

Kaaya na wachezaji hao watatu walizuiwa kuondoka na wenzao baada ya kukutwa na maambukizi ya Korona, kufuatia vipimo walivyofanyiwa saa chache baada ya kuwasili Angola, walipokwenda mjini Luanda kucheza mchezo wa hatua ya 32 Bora dhidi ya Primeiro De Agosto, ambapo hata hivyo mchezo huo haukufanyika.

Mapema leo mchana kongozi na wachezaji hao waliweka video kwenye mtandao wa Instagram ambayo inathibitisha kuruhusiwa kutoka ‘KARANTINI’, na kuwa tayari kuanza safari ya kurejea nyumbani kujiunga na wenzao.

Bado haijafahamika kama wachezaji wa Namungo FC na kiongozi wao watarejea nchini kwa gharama za serikali ya Angola ama gharama za klabu hiyo yenye maskani yake makuu mjini Ruangwa mkoani Lindi.

Mwenyekiti wa Namungo FC Hasan Zidadu alipozungumza na waandishi wa habari juma lililopita alisema gharama za kurejea kwa kiongozi na wachezaji watatu waliokua wamezuiwa nchini Angola zitabebwa na Serikali ya Angola.

Hata hivyo Namungo FC inaongoza mabao sita kwa mawili dhidi ya Primeiro De Agosto, na sasa inasubiri mchezo wa mkondo wa pili ambao utachezwa kesho alhamisi (Februari 25) nchini Tanzania kwa maagizo yaliyotolewa na Shirikisho la soka Barani Afrika.

Namungo FC endapo itapata matokeo ya jumla dhidi ya Primeiro De Agosto itafuzu kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho la Soka Barani Afrika.

Tayari makundi ya michuano hiyo yameshapangwa na mshindi wa mchezo kati ya Naumgo FC dhidi ya Primeiro De Agosto amepangwa katika kundi D lenye timu za Raja Casablanca (Morocco), Pyramid (Misri) na Nkana FC (Zambia).

2021 AFCON U17: Tanzania yapangwa kundi B
Magufuli apanga kulivunja jiji la Dar es Salaam