Hatima ya makada waandamizi wa CCM, Abdulrahman Kinana, Yusuf Makamba na Bernard Membe imewekwa kiporo na kamati kuu ya chama hicho hadi ripoti itakapokamilika ndani ya siku saba.

Akizungumza na waandishi wa habari, katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Humphrey Polepole amesema kikao cha kamati kuu kilichokaa chini ya mwenyekiti wao Rais, John Magufuli kimetoa muda huo kwa kamati ndogo ya udhibiti na nidhamu kukamilisha taarifa inayowahusu wanachama hao watatu na kuwasilisha katika vikao husika.

Wanasiasa hao walihojiwa kwa nyakati tofauti Dodoma na Dar es salaam kutokana na kutuhumiwa kwa makosa ya kimaadili baada ya mkutano wa Halmashauri kuu uliofanyika Desemba 13 mwaka jana jijini Mwanza kuazimia waitwe na kuhojiwa.

Vigogo hao wamehojiwa na kamati ndogo ya maadili chini ya makamu mwenyekiti wa CCM Bara, Philip Mangula baada ya sauti zao kusambaa katika mitandao ya kijamii wakieleza jinsi CCM ilivyopoteza mvuto na jinsi chama kilivyoshindwa kuwalinda makatibu hao dhidi ya mwanaharakati ambaye alikuwa akitoa tuhuma dhidi yao.

Sauti hizo zilianza kusambaa mitandaoni baada ya kinana na Makamba kuandika waraka Julai mwaka jana kwenda kwa katibu wa baraza la wazee CCM, Pius Msekwa wakidai uongozi hauwalindi dhidi ya mtu huyo ambaye walidai anawadhalilisha na huenda alikuwa analindwa na mtu mwenye mamlaka.

Vigogo hao walikitumikia chama hicho kwa nyakati tofauti ikiwa watapatikana na hatia watakabiliwa na adhabu mbili kwa mujibu wa kanuni za uongozi na maadili za CCM toleo la mwaka 2017 ikiwa watapatikana na hatia.

TMA: Tahadhari ya mvua kubwa kwa siku tano
Joseph Shabalala mkali wa miondoko ya kizulu afariki dunia