Mshambuliaji hatari wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Kipre Tchetche, ameweka rekodi ya kufunga hat-trick ya kwanza kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF) mwaka huu baada ya jana kufunga mabao matatu katika ushindi wa timu hiyo wa 4-3 dhidi ya Bidvest Wits ya Afrika Kusini, mchezo uliofanyika Uwanja wa Azam Complex,Chamazi jijini Dar es Salaam.

Hat-trick hiyo pia imemfanya Tchetche kuweka rekodi nyingine ya kutupia mabao matatu kwa mara ya kwanza kwenye ardhi ya Tanzania na michuano ya CAF tokea alipojiunga na Azam FC mwaka 2011 akitokea Jeunesse Club d’Abidjan Treichville (JCAT) ya kwao Ivory Coast.

Kihistoria hiyo ni hat-trick yake ya pili kwenye soka la ushindani, ya kwanza akiifunga alipokuwa JCAT walipocheza na Bingerville (4-0) katika ligi ya kwao, yeye akifunga mabao yote manne.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu hii wa www.azamfc.co.tz Tchetche alisema ana furaha kubwa kufunga mabao hayo huku akidai kuwa amekuwa akijitahidi sana kila mara kujituma na kufanya vema uwanjani.

“Sina cha kusema sana, ila ni muendelezo wa kujituma uwanjani kwa ajili ushindi na kupata matokeo mazuri kwenye mechi,” alisema.

Tchetche mpaka sasa kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) ameshafunga mabao tisa akiwa ndiye mfungaji kinara wa Azam FC akifuatiwa na nahodha John Bocco ‘Adebayor’ na Shomari Kapombe wenye mabao nane kila mmoja.

Picha: Magufuli atekeleza agizo la Makonda, awasilisha silaha yake
Hatma Ya Patrick Liewig Ipo Mikononi Mwa Viongozi Wa Stand Utd