Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji ya Ligi Kuu ya Bodi ya Ligi ‘TPLB’ imemkuta na Hatia ya Utovu wa Nidhamu Mshambuliaji wa klabu ya Coastal Union Maabad Maulid Maabad, kuptia mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Azam FC.

Miamba hiyo iliyokutana Jumapili (Novemba 27) katika Uwanja wa Azam Complex-Chamazi jijini Dar es salaam, ambapo Mshambuliaji Maabad aliitanguliza Coastal Union kwa kuifungia bao la kuongoza.

Hata hivyo Maabad alionekana akilumbana na Mwamuzi wa mchezo huo mara baada ya mchezo kumalizika, kwa kisingizio cha kuchukizwa na maamuzi ya kuongeza muda, ambao unatajwa kuibeba Azam FC kupata bao la ushindi dakika lala salama.

Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji ya Ligi Kuu ya Bodi ya Ligi ‘TPLB’ imetangaza kumfungia Mshambuliaji huyo kutoka Visiwani Zanzibar Michezo mitatu na kutozwa Faini ya Shilingi Laki Tano (500,000) kwa kosa kumshambulia Mwamuzi wa Kati kwa kumrushia chupa ya maji na baadae kiatu.

Maabad ambaye alikua katika Benchi la Ufundi baada ya kufanyiwa mabadiliko, alionekana akiingia Uwanjani na kumrushia chupa Mwamuzi wa Kati wakati mchezo ukiendelea, kisha kwenda kumshambulia Mwamuzu huyo kwa kutumia kiatu, baada ya mchezo kumalizika.

Adhabu hiyo dhidi ya Maabad imetolewa kwa kuzingatia Kanuni 41:5 (5.3) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji.

Wakati huo huo Klabu ya Coastal Union imetozwa Faini ya Shilingi Milioni Moja (1,000,000) kwa kosa la baadhi ya Wachezaji na Viongozi Benchi la Ufundi kurusha Chupa za maji Uwanjani wakati mchezo wao dhidi ya Azam FC ukiendelea.

Adhabu hiyo dhidi ya Klabu ya Coastal Union imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 47:1 ya Ligi Kuu kuhusu udhibiti wa Klabu.

Nayo Klabu ya Azam FC imetozwa Faini ya Shilingi Milioni Moja (1,000,000) kwa kosa la shabiki wake aliyekua ameketi kwenye jukwaa la watu maalum kurusha chupa ya maji kwa hasira katika eneo hilo, baada ya timu ya Coastal Union kupata bao la kusawazisha.

Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 47:1 ya Ligi Kuu kuhusu ushibiti wa Klabu.

Okwa arejea kundini Simba SC
Nasreddine Nabi kuikosa Tanzania Prisons