Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro amesema mwelekeo wa Serikali katika kukiendeleza Kiswahili unafanya Mahakama kutembea ‘kifua mbele’ kwa kuzingatia usemi wa kuthamini mali yako.

Dkt. Ndumbaro, amesema hayo Julai 4, 2022 katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam wakati anapokea maandamano ambayo yanahusu Kiswahili na haki kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Utamaduni Duniani (MASIKIDU).

“Kiswahili chetu tu, ndicho tunachopaswa kujivunia kila siku, lugha za wengine siyo zetu. Kwa hiyo, Kiswahili ndiyo lugha pekee ambayo imetufanya Watanzania kwa miaka sitini ya uhuru, kuishi pamoja na kufanya shughuli zetu kwa undugu, utulivu, amani na umoja,” amesema Dkt Ndumbaro.

Amesema, hatua hiyo imekifanya Kiswahili kupigiwa upatu na kutumika katika masuala yote ya kisheria ikiwa ni pamoja na kanuni zake zote, ambapo Mahakama ya Tanzania kama mdau wa Kiswahili inaamini uamuzi unaofanywa na serikali ni wa kizalendo.

Ameongea kuwa, hatua hiyo itawawezesha Watanzania na wananchi kupata fursa za kushiriki katika shughuli za ukalimani, tafsiri, uhariri, uandishi na uchapishaji wa vitabu vya sheria kwa Kiswahili.

Aidha, Dkt. Ndumbaro ameigiza Wizara ya Katiba na Sheria kushirikiana na Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA), na Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA,) kuendelea kutafsiri Sheria na Kanuni zote kwa Kiswahili ili wananchi wawe na nafasi ya kupata uelewa wa mwenendo wa kesi zao.

Hata hivyo, Dkt. Ndumbaro amesema kuna utaratibu wa kuwa Mahakama za kimtandao na kutafuta programu ya akili bandia ambao ni mfumo wa kutafsiri na kuandika taarifa za mashauri mahakamani kwenye lugha zaidi ya kumi ikiwamo lugha ya Kiswahili.

Naye Katibu Mtendaji wa BAKITA, Consolata Mushi amesema kuwa Tanzania ndiyo asili ya Kiswahili ambapo Kiswahili kinatumika kutoka kunakucha hadi kunakuchwa, watu wanaitumia lugha hiyo katika kutekeleza majukumu yao kitaifa, kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Serikali kuimarisha uwekezaji, biashara na utalii
Simba SC yakaa mguu sawa