Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemtaka mwenyekiti wa kampuni inayoshughulikia uwekezaji wa mitaji na dhamana (Egma), Harry Kitilya na wenzake kuwa na imani pamoja na subira dhidi ya upelelezi wa kesi ya utakatishaji fedha inayowakabili kwa kuwa unakaribia kufika mwisho.

Hayo yamesemwa hii leo Jijini Dar es salaam na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Cyprian Mkeha ambapo amewataka kuwa wavumilivu kwa kipindi hiki ambacho upelelezi ukiendelea.

Aidha, kabla ya Hakimu Mkeha kusema hayo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Kishenyi Mutalemwa amesema kuwa mara ya mwisho waliomba siku 14 ili waweze kuelezea hali ya upelelezi ulipofikia lakini wameshindwa hivyo wakaomba kuongezewa muda ili tarehe ijayo waweze kueleza.

Kwa upande wake Wakili wa utetezi, Masumbuko Lamwai amedai kuwa kesi ilifikishwa mahakamani hapo Aprili Mosi, 2016, hivyo ni karibu mwaka mmoja na nusu sasa, mashtaka yanayowakabili wateja wake yanahusisha nyaraka ambazo wanazo na kwamba hakuna uchunguzi nje ya nyaraka.

“Hii kesi imekuwa kama ya kukomoana komoana hivi, mheshimiwa wateja wetu ni watu wazima wanashughuli zao na nyingine zimefilisika kwa kukosa usimamizi,” amesema Wakili Lamwai mahakamani hapo.

Hata hivyo, Baada ya kutolewa kwa maelezo ya pande hizo zote mbili, Hakimu Mkeha amewaambia washtakiwa kuwa upelelezi unaofanywa unakaribia mwisho akaomba wawe na imani, kwa kuwa amejiridhisha yeye mwenyewe kwa macho yake kuwa upelelezi unakaribia kufika mwisho.

Wafahamu Marais tajiri Afrika
Ibrahim Akilimali ashtukia mgomo wa wachezaji