Wakati joto la pambano la masumbwi kati ya bondia ambaye hajawahi kuonja kushindwa, Floyd Mayweather na bingwa wa mapigano ya UFC, Conor McGregor linazidi kupanda, kituo kitakachoonesha pambano hilo kimewekwa wazi.

Vituo vyote vya runinga vya Sky Sports na mifumo yake ya kidijitali ikiwemo Sky Sports Box Office imetajwa kuwa ndio itakayoonesha rasmi pambano hilo kwa mamilioni duniani.

Kwa watakaoangalia pambano hilo litakalofanyika katika ukumbi wa T-Mobile Arena Las Vegas Marekani, tarehe 26 mwaka huu, kupitia Sky Sports Box Office watatakiwa kulipia kiasi cha £19.95 (sawa na shilingi 59,000 za kitanzania).

Mayweather ambaye anarekodi nzuri ya kushinda mapambano yake yote 49 anapewa nafasi kubwa ya kushinda pambano hilo huku McGregor akiendelea kusisitiza kuwa ataishangaza dunia katika siku hiyo na kumuwekea doa bingwa huyo wa zamani wa masumbwi.

Wapiganaji hao wanaendelea na ziara yao ya kulitangaza pambano lao katika majiji mbalimbali nchini Marekani. Pambano hilo linatajwa kuvunja rekodi ya dunia ya mauzo ya tiketi na idadi ya watu watakaolishuhudia kupitia mfumo wa ‘pay-per-view’.

Dk. Ndumbaro, Mgongolwa Wateuliwa TFF
Video: Waziri Mkuu atembelea kiwanda cha kampuni ya SBC Tanzania Ltd