Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans Nasreddine Mohamed Nabi amefurahishwa na ujio wa Mlinda Lango Metacha Boniface Mnata, ambao umeonekana kumpa changamoto mpya Mlinda Lango chaguo la kwanza klabuni hapo Djigui Diarra.

Metacha ni kati ya wachezaji wapya waliosajiliwa kupitia Usajili wa Dirisha Dogo uliofungwa rasmi Januari 15, 2023. Wengine ni Mashambuliaji Kennedy Musonda (Zambia), Beki Mamadou Doumbia (Mali) pamoja na Kiungo Mudathir Yahya Abbas (Zanzibar).

Akizungumza jijini Dar es salaam Kocha Nabi amesema kwa namna alivyomuona Metacha mazoezini, anaamini ataleta jambo jipya kwenye kikosi chake kwa kumpa changamoto Diarra.

Amesema ujio wa Mlinda Lango huyo mzawa utaimarisha kikosi chake kuelekea Hatua ya Makundi Kombe la Shirikiso Barani Afrika, Ligi Kuu Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho ‘ASFC’.

“Ninafurahi namna Metacha anavyomchalenji Diarra, hivyo ndivyo nilivyokuwa ninataka kwani niliwaambia viongozi nahitaji kipa wa kumpa changamoto Diarra.”

“Akiwepo kipa wa kiwango kidogo, kutamfanya Diarra abweteke na kiwango chake kushuka, hivyo Metacha atampa changamoto kwa sasa.”

“Katika Kikosi changu nahitaji wachezaji wa kuwapa changamoto wale waiojihakikishia nafasi kwenye kikosi cha kwanza.” amesema Nabi

Metacha aliwahi kuitumikia Young Africans misimu miwili iliyopita, lakini aliondoka Klabuni hapo baada ya kuonesha utovu wa nidhamu kwa mashabiki wa klabu hiyo, ambao walichukizwa na kiwango chake wakati wa mchezo dhidi ya Ruvu Shooting msimu wa 2020/21.

Ibenge: Young Africans haina sababu ya kushindwa
Wizara yafafanua kifo cha Mtanzania nchini Urusi