Meneja wa Klabu ya Liverpool, Jurgen Klopp amedai kuwa kushindwa kujipatia alama tatu muhimu dhidi ya Leicester City jana, kulichangiwa na theluji iliyotanda juu ya anga la Anfield.

Ameeleza kuwa kutokana na hali hiyo ya hewa, ilikuwa vigumu kwa washambuliaji wake kukokota vyema mpira na kupachika magoli, ingawa waliongoza kwa mbali kwa kumiliki mpira.

“Uliona hiyo, mpira ulikuwa haukokoteki vizuri. Kama ulikuwa na mpira kwa wastani wa 70% na 80% ya muda wote, inafanya maisha yanakuwa magumu na kukosa amani,” alisema Klopp.

Kadhalika, Klopp alimtupia lawama muamuzi kwa kutowapa penati baada ya Naby Keita kuchezewa ndivyo sivyo na mchezaji wa Leicester City, Ricardo Pereira akiwa ndani ya 18.

Naby Keita akienda chini baada ya kuchezewa ndivyo sivyo na Ricardo Pereira ndani ya eneo la 18. 

Liverpool ilijiongezea alama moja na kuendelea kukaa kileleni, baada ya matokeo ya sare ya 1-1 kwenye mechi hiyo ya Ligi Kuu ya Uingereza.

Matokeo hayo yanaipa shaka Liverpool kwa kusogea alama 5 zaidi ya Manchester City inayowanyemelea kwani wengi waliamini baada ya mchezo wa jana ingetengeneza utofauti wa alama 7.

Hata hivyo, Kocha Mhispania, Pep Guardiola amesema hana matumaini ya kunyakua kombe hilo kwani anaona kasi ya Liverpool wakati wao wakipoteza juzi dhidi ya Newcastle 2-1.

Liverpool imeandika rekodi ya alama 61 mbele ya Manchester City yenye alama 56 na Tottenham yenye alama 54.

Lema ajitosa sakata la Lissu, 'niko tayari kujiuzulu'
Mahakama Kuu yawaita Zitto, Spika Ndugai