Kikosi cha KMC FC kimekamilisha maandalizi yake ya mwisho leo Jumatatu (Oktoba 18) kuelekea mchezo wa Ligi kuu Tanzania utakaowakutanisha dhidi ya Young Africans, utakaopigwa kesho Jumanne (Oktoba 19), Uwanja wa Majimaji Songea mkoani Ruvuma.

KMC FC ambayo ni mwenyeji wa mchezo huo, imejizatiti kuutumia vyema uwanja wa nyumbani ili kupata matokeo mazuri ikiwa ni pamoja na kuondoka na alama tatu.

Timu hiyo ya Manispaa ya Kinondoni ambayo iliwasili mjini Songea siku ya Ijumaa (Oktoba 15) imekuwa na wakati mzuri wa kufanya mandalizi tangu ilipokuwa Jijini Dar es Salaam na hata ilipowasili mjini humo, ambapo hadi sasa wachezaji wote wapo vizuri kiafya na kiakili.

KMC FC chini ya kocha mkuu John Simkoko na wasaidizi wake Habibu Kondo na Hamad Ally inatambua ushindani uliopo katika mchezo huo lakini wachezaji, benchi la ufundi wamejidhatiti vizuri kuwakabili wapinzani wao.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya KMC FC Christina Mwagala amesema: “Ligi ni ngumu na inaushindani mkubwa kwa kila Timu unayokutana nayo, lakini KMC FC tumekuwa na maandalizi mazuri na kwamba yamekamilika kwa asilimia kubwa tangu tulipokuwa Dar es Salaam, kwasababu mchezo huu ulikuwa unafahamika kuwa upo kwenye tariba ya michezo yetu kwa mujibu wa Bodi ya Ligi, hivyo tumejipanga kushinda.”

“Kikubwa mashabiki wetu wajitokeze kwa wingi uwanjani ili kuwapa sapoti wachezaji wetu, mechi ipo ndani ya uwezo wetu, KMC FC tumekuja Songea kutoa burudani ya kipee na kwa kulitambua hilo tunakwenda kupambania alama tatu, sisi ndio wenyeji wa mchezo hivyo kila kitu tumekamilisha vizuri kuanzia upatikanaji wa Tiketi bila kuwepo kwa changamoto yoyote.”

KMC FC mpaka sasa ina alama moja baada ya kuambulia sare ya bila kufungana dhidi ya Coastal Union huku wakipoteza mchezo wao wa kwanza dhidi ya Polisi Tanzania walioibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Kwa upande wa Young Africans wamejikusanyia alama 6, baada ya kuzichabanga Kagera Sugar na Geita Gold bao 1-0 kila mmoja katika michezo ya mzunguuko wa kwanza na wapili.

Longido yaneemeka
UVIKO 19 chanzo cha Ukosefu wa Ajira na Wimbi la Umasikini