Baada ya kuanza kwa kusasua Msimu Mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Kocha Mkuu wa KMC FC Hitimana Thierry, amesema anautumia vyema muda huu wa mapumziko kukiimarisha kikosi chake na hatimaye kurejea Dimbani kikiwa na nguvu mpya.

KMC FC ilianza msimu mpya kwa kufungwa na Coastal Union 1-0, na mchezo uliofuata ililazimishwa sare ya 2-2 dhidi ya Polisi Tanzania.

Hitimana amesema baada ya kutofanya vizuri katika michezo hiyo waliocheza ugenini Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, alibaini safu yake ya ulinzi ilikuwa na mapungufu, ambayo sasa ameyafanyia kazi kwa ajili ya kupata ushindi kwenye michezo miwili inayofuata.

“Msimu uliopita tulikuwa na tatizo la Beki wa Kati, tumefanya usajili katika eneo hilo, naendelea kutengeneza muunganiko mzuri wa kikosi kwa kuboresha kuanzia safu ya Ulinzi, Viungo na Ushambuliaji,”

“Tunatumia mapumziko haya kucheza michezo ya kirafiki ili kujiweka vizuri na tutakaporejea katika ligi, tunahitaji kuja kivingine zaidi kwa kupata ushindi katika michezo iliyo mbele yetu ukiwemo mchezo dhidi ya Simba SC.” amesema hitimana

Ameongeza wamejiandaa kucheza kwa tahadhari katika mchezo dhidi ya Simba SC, huku akisifia kikosi alichokisajili kwa kusema kitasaidia kumpa matokeo chanya.

KMC FC itakua mgeni wa Simba SC katika Uwanja wa Benjamin Mkapa siku ya Jumatano (Septemba 07).

Serikali yaainisha fursa za uwekezaji sekta ya Madini
Wataalamu wa Afya wahimizwa uwajibikaji, uadilifu