Nyota wa zamani wa timu ya Lakers ya ligi ya mpira wa kikapu ya NBA ya Marekani, Kobe Bryant amefariki dunia kwa ajali ya helikopta, Jumapili, Januari 26, 2020.

Bryant aliyekuwa na umri wa miaka 41 alikuwa akisafiri kwa kutumia helikopta binafsi akiwa na watu wengine wanne, lakini chombo hicho kilianguka katika eneo la Calabasas, California.

Polisi wa Los Angeles wamethibitisha kifo cha Bryant na wenzake wanne na kwamba uchunguzi juu ya chanzo cha ajali hiyo unaendelea. Pia, wamethibitisha kuwa mkewe Vanessa hakuwa miongoni mwa watu hao.

Los Angeles Times wameripoti kuwa helikopta ilikita katika ukingo wa mlima na kushika moto.

“Kwa majonzi makubwa, tunasikitika kutangaza kifo cha Kobe Bryant na watu wengine wanne kwenye ajali ya helikopta iliyotokea Calabasas. Chombo hicho cha usafiri wa anga kilianguka majira ya saa nne asubuhi. Hakuna mtu aliyekuwa chini/ardhini aliyeumia. Vyombo vyetu vya FAA na NTSB vinaendelea na uchunguzi,” imeeleza taarifa rasmi ya jiji la Calabasas iliyowekwa pia kwenye akaunti yao ya Twitter.

Bryant aliichezea Lakers ya Los Angeles kwa kipindi chote alichocheza ligi ya NBA, ikiwa ni tangu mwaka 1996 hadi 2016 na alifanikiwa kuisaidia kushinda mataji matano ya ubingwa wa NBA.

Alistaafu kucheza mpira wa kikapu akiwa na alama 33,643, ambazo ziliingia kwenye rekodi katika nafasi ya tatu katika historia yote ya mchezo huo.

Rekodi hiyo ilisimama hadi Jumamosi, Januari 25, 2020 baada ya LeBron James kuipita akifikisha alama 33,644 ya upachikaji wa magoli.

Jumapili, majira ya saa kumi na mbili na dakika 39, ikiwa ni saa nne tu kabla ya kifo chake, Bryan alitweet akimpongeza James kwa kuvunja rekodi yake.

“Endelea kuupeleka mbele huu mchezo @KingJames heshima kubwa kwako kaka #33644,” tafsiri isiyo rasmi ya tweet ya Bryant kuhusu LeBron anayetumia @KingJames kwenye Twitter.

Kobe Bryant akiwa na LeBron JamesBryan alifunga ndoa na Vanessa mwaka 2001 na walifanikiwa kupata watoto wanne.

Moja kati ya nukuu zake bora ni, “kila kitu hasi-changamoto, misukumo-hiyo kwangu ni fursa ya kuendelea kupanda.”

Nukuu nyingine ni “nitafanya kila kitu kuhakikisha timu yangu inashinda, iwe ni kukaa kwenye benchi na kupunga taulo, kumpa kikombe cha maji mchezaji mwenzangu au kuingia uwanjani na kufunga magoli.”

Serikali kuendelea kuzuia mikutano ya kisiasa isiyofuata sheria
Tanzania, India kuendeleza uhusiano wa kidiplomasia, kukuza maendeleo

Comments

comments