Mshambuliaji Nicklas Bendtner ameondolewa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Denmark kitakachokwenda Urusi kushiriki fainali za kombe la dunia, zinazotarajiwa kuanza Juni 14.

Bendtner ameachwa kwenye kikosi cha mwisho cha wachezaji 23 wa nchi hiyo, kufuatia majeraha nyonga alioyapata akiwa katika klabu yake ya Rosenborg ya Norway juma moja kabla ya kujiunga na kikosi cha Denmark.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 30, alijaribu kufanya mazoezi na kikosi cha Denmark na kuonyesha maendeleo mazuri, pia alipata nafasi ya kucheza mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Sweden mjini Stockholm, juzi jumamosi.

Jana jumapili alifanyiwa mtihani wa mwisho wa upimaji wa afya, lakini hakuwaridhisha madaktari wa timu ya taifa ya Denmark na kupelekea kocha mkuu Age Hareide kumuacha sambamba na beki Andreas Bjelland.

“Hatuamini kama wataweza kuwa FIT kabla ya mchezo wetu dhidi ya Peru, tumewajaribu na imeonyesha hawapo katika hali nzuri ya kwenda kupambana katika fainali za kombe la dunia,” Alisema Hareide kupitia video iliyowekwa kwenye ukurasa wa Twitter wa chama cha soka nchini Denmark.

“Tulitamani sana kuwajumuisha kwenye kikosi chetu, lakini imetulazimu kuwaacha ili waweze kupata nafasi ya kupona vizuri.” Aliongeza Hareide.

Umahiri wa Bendtner ulianza kuonekana akiwa na klabu ya Arsenal na baadae Juventus, huku upande wa timu ya taifa makeke yake yalionekana wakati wa mchezo wa kombe la dunia mwaka 2010 baada ya kufunga bao la kwanza dhidi ya Cameroon waliokubali kufungwa mabao mawili kwa moja.

Katika fainali za mwaka huu, Denmark itakutana na Peru, Australia na Ufaransa katika michezo ya kundi C.

Luka Modric: Neymar tunakusubiri
Urusi 2018: Nani atabeba Kombe? Tuimulike Serbia