Siku chache kabla ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa hatua ya Makundi utakaochezwa jijini Dar es salaam, Uwanja wa Benjamin April 03, kocha mkuu wa AS Vita Florent Ibenge ametuma salamu kwa wapinzani wao Simba SC.

Ibenge ambaye bado anakumbuka kilichomfika kwenye michuano hiyo mwaka 2019 alipocheza dhidi ya Simba SC uwanjani hapo kwa kufungwa mabao 2-1, amesema kuna ulazima wa kikosi chake kufanya jitihada za kushinda mpambao ujao dhidi ya mabingwa hao wa Tanzania Bara, ili kufikia lengo la kusonga mbele kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kocha huyo kutoka DR Congo amesema ili AS vita iweze kusonga mbele katika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika inatakiwa kuibuka na ushindi katika michezo yao miwili iliyosalia ya ligi hiyo, dhidi Simba na Al Merrikh.

Amesema kuwa kulingana na matokeo na alama ambazo wamezipata wanatakiwa kushinda michezo yao miwili ijayo bila kujali wanakutana na timu ipi kwani wasipofanya hivyo hawatakuwa na uwezo wa kusonga mbele kuelekea katika hatua ya robo fainali.

“Tunatakiwa kushinda michezo yetu yote miwili iliyosalia dhidi ya Simba na Al Merrikh ili tuweze kusonga mbele katika hatua ya robo fainali, matokeo tuliyopata hayakuwa mazuri sana kwetu lakini huu si muda wa kulaumiana tunachotakiwa kufanya ni kuhakikisha tunasonga mbele.

“Tunatakiwa kutojali tunacheza na mpinzani wa aina gani, michezo yote iliyosalia ni migumu kwetu tunacheza na Simba tukiwa ugenini mara ya mwisho tulipoteza mchezo pale hivyo hatutakiwa kurudia makosa, mchezo wa mwisho tutakuwa nyumbani kila mtu anafahamu hatujashinda hata mchezo mmoja kwetu pia tunatakiwa kurekebisha hili,” amesema kocha Ibenge.

AS Vita kwa sasa inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ‘Kundi A’ la Ligi ya Mabingwa Barani Afrika mara baada ya kujikusanyia alama 4 nyuma ya Simba wenye alama 10 na Al Ahly wana alama saba.

Rais Xi Jinping wa China amlilia Hayati Dkt Magufuli
Mkwasa aahidi mazito Ligi Kuu